Na Saleh
Ally
ZOEZI la
usajili katika Klabu ya Simba linaongozwa na Zacharia Hans Poppe, mwanajeshi
mstaafu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Msimbazi.
Kamati ya
Hans Poppe ambayo makamu wake ni Kassim Dewji ndiyo ilifanya usajili ambao
uliaminika ni bora, lakini katika mechi saba za Ligi Kuu Bara, ilitoka sare
sita na kushinda moja!
Hali hiyo
iliashiria kutofanyika vizuri kwa usajili na sasa kamati hiyo imekuwa ikifanya
usajili kuhakikisha inarekebisha mambo. Katika mahojiano maalum na Championi
Ijumaa, Hans Poppe anafunguka wazi kwa kila swali.
Mgambia:
Kiungo
mshambuliaji Omar Mboob kutoka Gambia ametua nchini kwa ajili ya majaribio,
ikitokea amefuzu yupi kati ya Amissi Tambwe na Pierre Kwizera ataachwa?
Kwanza
nianze kuelezea kuhusiana na huyo Mgambia, nilikutana na wakala wake yuko huko Hispani.
Akasisitiza aje afanye majaribio akiamini ana uwezo mkubwa pia ni aina ya
mchezaji anayeweza kucheza barani Ulaya.
Tumekubali,
tumempa nafasi ya kumuona ila mawili yatatokea. Kutegemeana na uzuri wake,
ukiwa wa kawaida, basi atasubiri msimu ujao kwenye usajili mkubwa.
Akiwa mzuri
na tunaona atatusaidia, kweli tutahitaji nafasi moja. Mwalimu (Patrick Phiri)
ndiye ataamua kati ya Tambwe na Kwizera, kwamba nani aende. Maana kweli Simba
tunahitaji offensive midfield (kiungo mshambulizi) aliyeiva.
Kiongera:
Kiongera
mmemuacha, nafasi yake inachukuliwa na Danny Sserunkuma. Vipi mmevunja mkataba
kwa kutumia mfumo upi?
Kwanza
nifafanue, hatujavunja mkataba na Kiongera. Bado yuko chini yetu, sisi ndiye
tunaogharimia matibabu yake, pia tutaendelea kumlipa mshahara hadi hapo
atakaporudi maana tunamhitaji, tatizo limekuwa ni majeraha tu.
Mapumziko
yake ni marefu baada ya kutibiwa, zaidi ya miezi mitatu. Hatuwezi kuendelea
kuifunga nafasi wakati tunaihitaji, hivyo tumekubaliana vizuri na yeye
ameleelewa.
Chanongo:
Bado
haijajulikana, taarifa zinaeleza Haruna Chanongo anatakiwa na Mtibwa Sugar,
lakini wako wanasema Simba inamshusha timu B, wewe kama bosi wa usajili, ukweli
hasa ni upi?
Wakati
mwingine naona kama Chanongo mpira wake kama ndiyo umefikia hapo. Nimewahi
kuzungumza naye kama mzazi mara kadhaa, nilimueleza namna anavyoshindwa kufanya
uamuzi kila anapoingia kwenye 18 ya adui.
Hauwezi
kuwa mchezaji uko kwenye lango la adui, unarudisha mpira kwa namba tatu wenu.
Hii imefanya hadi watu waanze kuamini anaihujumu timu, inaweza isiwe hivyo.
Mchezaji
gani asiyebadilika, angalia Simba tulivyompa nafasi tukionyesha tunamuamini. Nimesikia
hata alipoitwa kuzungumza na viongozi alionyesha utovu wa nidhamu wa hali ya
juu.
Sikuwepo,
nilikuwa safari. Nimesikia anarudishwa kikosi B. Lengo akajifunze zaidi,
ikishindikana basi. Nimesikia wakala wake anataka aachiwe aende, sasa sijajua
hili limeishia wapi hadi sasa.
Unajua kuna
timu zinamtaka kwa mkopo, sheria ya mkopo sisi ndiyo tumlipe. Sasa kama
tunamlipa sisi, kuliko kuwa kwenye timu nyingine, basi bora acheze timu ya
vijana ambako anaweza kubadilika.
Kessy:
Kuna
taarifa mnataka kumsajili beki wa kulia wa Mtibwa Sugar?
Hassan
Ramadhani ‘Kessy’, kweli huyu ni beki wa kulia wa Mtibwa Sugar. Tayari tumeanza
kuzungumza na uongozi wa klabu hiyo.
Nafikiri
hatuko pabaya na tayari walikuwa wametoa ofa na tunaifanyia kazi, ninaamini
baada ya siku mbili hizi tutakuwa naye kikosini.
Casillas:
Kuna taarifa za kwamba mnataka kumuacha kipa Cassilas?
Kwa kweli
suala hilo bado hakuna taarifa za uhakika kama anaachwa. Kikubwa ni kuangalia
matibabu yake na kamati ya utendaji ndiyo inaweza kuamua siku ya mwisho, hivyo
siwezi kutoa jibu la moja kwa moja.
Mechi 7:
Mlikosea
nini hasa katika usajili wa mwanzo wa msimu hadi timu ikapata sare sita katika
mechi saba?
Hatujawahi
kukaa tukafanya analysis (uchambuzi), lakini kama ni maoni yangu binafsi,
kikosi hakikuwa kibaya sana ingawa kweli tumefanya mabadiliko. Kambi ya
Zanzibar timu ilikuwa vizuri, tulipoanza ligi, mechi dhidi ya Coastal tulicheza
nzuri sana, tukafunga mabao mawili.
Mwamuzi wa
siku hiyo alianza kutuvuruga, bao la kwanza halikuwa sahihi. Bao la pili la
mkwaju wa adhabu, niliona si sahihi Ivo (Mapunda) kufungwa bao rahisi hivyo,
tukaondoka mchezoni. Baada ya hapo, hatukucheza vizuri na inaonekana tatizo ni
la safu ya ushambuliaji na si mabeki.
Tatizo:
Unaposema
tatizo ni washambuliaji, una maanisha Simba ina safu nzuri ya ulinzi na
imewaridhisha?
Nianzie na Isihaka
Hassan, naamini atakuwa ni mmoja wa mabeki bora kabisa Tanzania. Amefanya kazi
yake vizuri, lakini bado kiungo hakikuwa bora, safu ya ushambuliaji ndiyo
ilikuwa tatizo zaidi.
Kama kiungo
kinayumba, mabeki hawawezi kufanya vizuri na utaona katika mechi saba, mechi
moja tu ya Coastal ndiyo safu ya ulinzi iliruhusu mabao mawili. Nyingine safu
haikuruhusu hata bao moja, au tulifungwa moja.
Sasa, safu
ya ushambuliaji siku tumefungwa moja, kwa nini haikufunga mbili? Siku
tulifungwa mbili mbona haikufunga tatu? Ndiyo maana nasema ushambuliaji ni
tatizo kubwa.
Kingine sub
(ubadilishaji wachezaji) haukuwa mzuri, huenda kocha alikuwa ni mwenye hofu
kila wakati.
Sub za
Phiri:
Kivipi sub
za Kocha Phiri hazikuwa nzuri, unafikiri zilichangia kuwaangusha?
Kabisa,
naona kama alikuwa muoga wakati mwingine, hataki kuchukua risk (kujaribu). Sub
ile ya (Amri) Kiemba dhidi ya Prisons ndiyo ilitumaliza. Pia alikuwa akiangalia
mazoea, hata mchezaji anazembea, ila kwa kuwa amemzoea, basi lazima acheze.
Vipi wengine ambao lazima wapewe nafasi ili uwezo wao uonekane. Kwani (Peter)
Manyika tulimuona vipi kama isingekuwa kumpa nafasi na majukumu mazito?
Mnawapangia
timu makocha:
Kuna
taarifa mmekuwa mkiwapangia timu makocha na wewe ni mmoja wapo?
Hizo ni
hadithi tu, lakini wakati mwingine unaweza kumshauri kocha na baadaye yeye na
timu yake ya benchi la ufundi wakaamua.
Nitakutolea
mfano, ile mechi ya 3-3 na Yanga, hadi mapumziko tulikuwa tumefungwa tatu.
Tumeingia vyumbani, (Abdallah) Kibadeni akaanza kuwaambia wachezaji kwamba
tumeishafungwa bao tatu, basi zinatosha tusiruhusu nyingine, hivyo tu basi!
Mimi uvumilivu
ukanishinda, nikamueleza kocha kiungo cha Abdulhalim (Humud) na Chanongo,
kimekufa, wawape nafasi vijana. Wakaingizwa Said Ndemla na Gallas na wakafanya
kazi tukasawazisha hadi mwamuzi akamaliza mpira kabla ya dakika hazijaisha.
.jpg)









0 COMMENTS:
Post a Comment