Na Saleh Ally
MTANZANIA Idris Sultan amefanikiwa kuipa nchi
yetu sifa, ameshinda taji la Big Brother HotShots 2014 na kutwaa kitita cha
zaidi ya Sh milioni 510.
Hongera kwake, si fedha kidogo kwa mashindano
ya miezi miwili na robo tu, lakini amezidi kuwahamasisha watu kuwa Tanzania ina
vijana wenye vipaji.
Pamoja na heshima kubwa kwa taifa, suala au
gumzo ni fedha zake, atazifanyia nini? Zitamsaidia vipi au atazitumia vibaya
kupitia mgawo wa kijinga ili afulie?
Ukweli huu ndiyo wakati wa lawama kwa Idris,
huenda kila mmoja anataka apewe shukurani kwa kuwa aliwahi kumsaidia hiki au
kile au alishiriki kwenye ishu ile au hii ya kumsaidia ashinde.
Huu ndiyo wakati ambao Idris hapaswi kuwa muoga
hata kidogo, asihofie lawama kutoka kwa yeyote, badala yake aangalie anafanya
nini.
Hili namnong’oneza, (wewe msomaji unaweza
kuruka hapa)-bora ukubali lawama, maana usipoiheshimu Sh 100, ikapungua kwenye
Sh milioni 1, basi haiwezi kuitwa milioni moja, itakuwa Sh 999,900. Maana yake
hata hiyo Sh milioni 520 na ushee, inaweza kuyayuka kama ukijidai mtu wa bata
sana au msamalia mwema kama nanihii, umekwisha.
Hakika sijui Richard Bezuidenhout aliyeshinda
dola 100,000 (Sh milioni 170) alizitumiaje. Sijui kama aliingia kwenye mgawo wa
kijinga!
Dua mbaya na nzuri tayari ziko hewani, si kweli
wote wamefurahia ushinde. Wako waliofurahia na waliokasirika bila ya wewe
kujua. Muhimu chunga makundi haya matatu, maana yataugeuza mgawo wa fedha zako
kuwa wa kijinga kabisa!
Ndugu:
Kundi la ndugu ni kubwa, lakini unaweza
kuligawanya katika makundi mawili. Waswahili wanasema ndugu lawama, kila ndugu
hataki kukosolewa, kuhojiwa wala kunyimwa ili mradi ajue kipo.
Kundi la kwanza ni lile la wale walioshughulika
kumsaidia Idris, mfano kampeni kuhakikisha anashinda au kumuunga mkono tu.
Kundi la pili ni lile ambalo lilikuwa limekaa
kando, halikujua kuhusu Big Brother au kama lilijua, lilidharau Idris angeweza
kushinda.
Makundi yote mawili yana haki sawa hasa ukija
katika neno ndugu. Hapo ndiyo kuna shida, Idris ana zaidi ya Sh milioni 510
mkononi. Sasa kwa nini asiwape hata Sh milioni 5, kila ndugu!
Ninaamini kuna ndugu angelalamika hata kama
angepewa Sh milioni 10, maana anaona Sh milioni 500 na zaidi ni nyingi sana!
Huu ndiyo wakati wa lawama kwa Idris, wakati wa
kipimo cha uwezo wa kuamua, kutafakari na baadaye kusonga au aamue, asitafakari
na arudi nyuma.
Hii inaonyesha lazima akubali kugombana na
watu, asemwe, alaumiwe, lakini kikubwa aangalie kipi ni sahihi.
Sh milioni 500 ni ndogo sana na huenda zikawa
ndogo zaidi kuliko Sh milioni moja kama zitatumika bila mahesabu sahihi,
mpangilio wa uhakika na plani za kitaalamu.
Wapambe:
Hawa wapo tu, tayari sasa wako sehemu wanapiga
mazoezi ya ‘nyimbo’ za kumuimbia Idris.
Kwa lawama, hawatofautiani sana na ndugu ingawa
wenyewe hawana nguvu ya ule ‘undugu wa damu’, lakini wanaamini wana hakika.
Unakumbuka Idris aliwahi kupewa nauli ya kwenda
sehemu fulani na nanihii, halafu alipelekwa klabu na nanihii. Sasa akina
nanihii wote nao wanataka angalau wale bata maana mshikaji wao ana mamilioni.
Watamkubusha Idris maisha ni mafupi. Shauri yake!
Ukweli, akidhubutu tu akaingia mkenge na
kuwasikiliza, hapo ndiyo atajua wapambe nuksi, siku akikwama, wao ndiyo
watakuwa wa kwanza kumcheka wakimtangaza kuwa mjinga kuzidi watu wote duniani,
hapa pia, lazima akubali lawama. Potelea mbali.
Warembo:
Hawa ndiyo professional zaidi, wanajua wanataka
nini kwa watu wenye chochote kitu mkononi. Idris alikuwa mpiga picha tu, nani
alimjua, kwa nini wamjali?
Warembo wa mjini wengi wanajali kwenye kitu,
wako walioruka juu kufurahia ushindi wa Idris alipotangazwa kupitia runinga, si
kwamba wanaipenda sana Tanzania, wanafurahia ‘duka’ jipya limefunguliwa nchini,
wanajua watafanyaje.
Usisahau Idris ni kijana, hata kama atawaza
biashara ili kujiendeleza, usinidanganye ‘hatapoza’ moyo.
Anaupozaje? Mimi na wewe hatujui, lakini vema
akawa makini asije akaubwaga kabisa na mwisho akafulia.
Warembo wana kila njia, kamwe hawawezi
kushindwa kumfikia. Si kama zile enzi zetu za barua, halafu unachora kopa
kibao, kati zina mshale uliokatiza.
Siku hizi kuna Instagram, Whatsapp, Viber na
takataka kibao. Watamfikia tu, lakini usisahau kuna wanaume wanaishi jijii Dar
kwa ukuwadi tu, wapo, unabisha nini?
Wao pia watahitaji kamisheni yao, hapo ndiyo
wataanza kazi ya kuwatafutia wasichana njia zote za kumfikia kijana huyo wa Big
Brother. Inawezekana kwa kufanya urafiki na ndugu zake, rafiki zake lakini ili
mradi wamfikie ili waweze kugawana kijinga fedha zake.
Wanapenda kugawana kijinga na mwisho watamcheka
kwa ujinga. Yeye ndiye anaweza kuamua azigawe kijinga au akatae kuwa mjinga,
maisha yasonge mbele.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment