Kiungo mshambuliaji wa kutegemewa wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, ameshusha presha
kwenye timu hiyo baada ya kutua nchini tayari kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani
Jembe 2 itakayopigwa Jumamosi ya wiki hii.
Katika mechi
hiyo, Simba inatarajiwa kuvaana na watani wao wa jadi, Yanga.
Kiungo huyo, hivi
karibuni alizua hofu kubwa kwenye timu hiyo baada ya kuchelewa kujiunga na
wenzake katika maandalizi kutokana na tabia yake ya kuchelewa mara kwa mara
anaporejea nyumbani kwao Uganda.
Kwa mujibu wa
chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kiungo huyo alitua juzi
Jumatatu saa tano usiku akitokea kwao Uganda katika mapumziko na kupokelewa na
viongozi wa timu hiyo.
Chanzo hicho
kilisema, kiungo huyo alitarajiwa kuelekea Unguja, Zanzibar jana Jumanne kwa
ndege kwa ajili ya kuwahi kambi ya pamoja ya kujiandaa na mechi ya Nani Mtani
Jembe.
“Okwi ametua
tayari usiku wa Jumatatu saa tano, akitokea kwao Uganda alipokwenda kwenye
mapumziko baada ya ligi kuu kusimama.
“Mara baada ya
kutua hiyo juzi, leo (Jumanne) anatarajiwa kuelekea Zanzibar ilipoweka kambi
timu ikijiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe itakayopigwa Jumamosi hii kwenye
Uwanja wa Taifa,” kilisema chanzo hicho.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, alikiri staa huyo
kuwasili kambini Zanzibar jana mchana.
“Okwi ametua hapa
Zanzibar tayari na leo jioni amefanya mazoezi na wenzake, naamini atatusaidia,”
alisema Phiri.
0 COMMENTS:
Post a Comment