| EMERSON |
Kocha Mkuu wa Yanga,
Mbrazili, Marcio Maximo, amemshtukia kiungo wake mpya mkabaji, Emerson De
Oliviera kuwa ni mzito na kutakiwa kuufanyia kazi mwili wake ili ahakikishe anapata
wepesi.
Awali, ‘ugonjwa’ huo wa
uzito aliwahi kuwa nao mshambuliaji wa timu hiyo Mbrazili, Geilson Santos
Santana ‘Jaja’ licha ya kufanyishwa mazoezi magumu ili apunguze uzito huo.
Emerson yeye alitua
kuichezea timu hiyo wiki moja iliyopita akitokea nyumbani kwao Brazil, amesaini
mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Yanga.
Katika kuhakikisha kiungo
huyo anapunguza uzito, Maximo amemuandalia programu maalumu ya mazoezi uwanjani
pamoja na gym.
Katika mazoezi ya jana
Ijumaa asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Loyola, Mabibo jijini Dar es
Salaam, Maximo alimzuia kugusa mpira kiungo huyo huku akimtaka kufanya mazoezi
ya mbio fupi na ndefu uwanjani.
Programu hiyo, ilisimamiwa
na kocha msaidizi, Leonard Neiva raia wa Brazil ambaye alianza peke yake kwa
kukimbia kuuzunguka uwanja kabla ya kuchanganywa na akina Said Bahanuzi,
Hussein Javu na Khamis Thabiti ambao walikimbizwa kwa raundi kumi.
Wakati wakiendelea kukimbia,
Neiva alionekana kuwaongezea programu nyingine ya kuruka koni ndefu sita na
fupi tano zilizopangwa uwanjani hapo.
Neiva, pia alimtaka Emerson
na wenzake kukaa chini na kunyanyuka kwa haraka wakifuata mlio wa filimbi
aliyokuwa akiipuliza na baada ya zoezi hilo wachezaji walionekana kuchoka.
Wakati Emerson na wenzake
wakiendelea na programu hiyo ya mazoezi magumu, wengine walikuwa wakicheza
mpira wakisimamiwa na Maximo ambaye alionekana akiwanoa kwa mbinu mbalimbali.







0 COMMENTS:
Post a Comment