| KIKOSI CHA VILLA SQUAD... |
Uongozi wa Villa Squad
umeliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukiomba mechi zao zilizobaki
za Ligi Daraja la Kwanza zichezwe kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi
unaomilikiwa na jeshi.
Hiyo ni baada ya kutokea
fujo kwenye mechi yao dhidi ya Friends Rangers iliyochezwa wikiendi iliyopita
kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Idd Godigodi, alisema kuwa, kutokana na
fujo walizofanyiwa wachezaji na baadhi ya viongozi wao, basi hawataki kuutumia
uwanja huo tena kwa hofu ya usalama wao.
Godigodi alisema tayari
wameiandikia barua TFF kubadili uwanja huo na kuutumia huo wa jeshi kutokana na
polisi wanaopangiwa kulinda usalama Karume kuonekana kuzidiwa na mashabiki wa
timu mbalimbali wakiwemo wa Friends Rangers.
“Kutokana na fujo
mbalimbali walizofanyiwa wachezaji wetu Nurdin (Bakari), Taita (Godfrey) na
Redondo (Ramadhani Chombo), tumeona ni bora tubadili uwanja huu unaotumika kwa
ajili ya mechi za ligi na tuhamie Mabatini Mlandizi.
“Kikubwa hatutaki kuona hiki
kilichotokea kinaendelea kwa wachezaji na baadhi ya viongozi wetu wakifanyiwa
fujo, hivyo tayari tumewaandikia barua TFF kwa ajili ya kuwafahamisha,” alisema
Godigodi.







0 COMMENTS:
Post a Comment