Na Saleh Ally
UKIYAFUATA yale mambo ya ushabiki yanaweza kukupoteza
kabisa. Yanga na Simba wao ni watani, wanajuana wenyewe.
Mimi nataka kumzungumzia Danny Sserunkuma kitaalamu kwa
maana ya nilivyomuona uwanjani katika mechi chache tu alizoichezea Simba.
Ukiangalia katika mechi tatu za mwanzo, unagundua wakati
anakuja Simba, Sserunkuma raia wa Uganda alikuwa hana mazoezi ya kutosha lakini
bado alitaka kulazimisha kucheza kama ilivyozoeleka.
Ukweli kwa alivyokuwa akionekana kwa maana ya umbo,
utaona anakwenda anapungua ukilinganisha na alivyokuja akiwa anaonekana ana
umbo kubwa zaidi.
Kiuchezaji Sserunkuma anaweza kuwa mmoja wa
washambuliaji au viungo wachezeshaji, washambuliaji hatari sana ambaye kwa
wachezaji wanaochipukia wanaweza kujifunza kwake.
Ana mambo mengi sana wachezaji hapa nyumbani hawana na
inawezekana ni vigumu kuyaona kama utamtupia jicho la kishabiki.
Ila ninaamini kama atacheza Simba angalau misimu miwili
akiwa fiti, basi majibu ya ninachokisema yataonekana.
Kushoto / kulia:
Ni kati ya wachezaji wachache kwenye ukanda wa Afrika
Mashariki wenye uwezo mkubwa wa kuitumia miguu yote kwa ufasaha.
Ana uwezo wa kupiga mashuti, krosi na chenga kwa kutumia
miguu yote miwili, hii ni hatari kwa kila beki anayemkaba.
Utamuona anapokuwa na mpira ni mchezaji anayechanganya,
beki hawezi kujua anataka kufanya nini kati ya hivi vinne. Kusimama au kwenda,
kupiga pasi au shuti.
Angalia alivyo na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho
ziwe za chini au juu na zinafika sawia.
Langoni:
Sserunkuma ni mjanja sana akiwa eneo la lango la timu
pinzani na hufunga kwa kujiamini.
Uwezo huu tokea nimemuona akiichezea Simba, bado
haujakaa sawa kwa kuwa anaonekana hayuko fiti.
Katika baadhi ya picha za video akiwa Gor Mahia, hakika ni
hatari kwa kulichambua goli la timu pinzani.
Kubadili mchezo:
Makocha wanaita jicho la mwewe. Uwezo wa kuangalia
haraka na kubadili mchezo au kushitukiza.
Wakati wengine wakiangalia huku, wewe unajua huku ndiyo
salama na mchezo unabadilika. Muangalie vizuri Sserunkuma.
Utulivu kwenye boksi:
Huenda hata Ulaya kuna rundo la wachezaji hawana utulivu
kwenye boksi, ni tatizo kubwa kwenye mchezo wa soka.
Sserunkuma akiingia kwenye 18, huenda akawa mmoja wa
wachezaji hatari sana. Utakubaliana na mimi kama ulishuhudia fainali ya Kombe
la Mapinduzi Simba ikipambana na Mtibwa Sugar.
Utulivu wake unampa nafasi za mambo mawili makuu kwa
nafasi pia. Kutoa pasi atakavyo au kufunga atakavyo pia.







0 COMMENTS:
Post a Comment