Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Phiri, raia wa Zambia, amesema kuwa bado anaendelea
na maisha mengine nje ya soka, ingawa yupo katika michakato ya kuhakikisha
anapata timu ya kufundisha kwa kuwa soka ni sehemu ya maisha yake.
Kocha
huyo mwenye rekodi ya kuchukua ubingwa wa Tanzania bila ya kupoteza mchezo
wowote akiwa na kikosi cha Simba msimu wa mwaka 2009/2010, ‘alimwagwa’ na klabu
hiyo mwishoni mwa mwaka jana kutokana na timu yake kutokuwa na matokeo mazuri
katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza kutoka jijini Lusaka, Zambia, Phiri
aliweka wazi kuwa kwa sasa hana timu, anaendelea na majukumu mengine nje ya
soka, lakini jitihada zinafanyika kupata klabu ya ‘kuikochi’ na hilo
likikamilika kila kitu kitawekwa hadharani, huku akigoma kuelezea ishu ya
malipo yake na Simba.
Mzambia
huyo aliongeza kuwa, amefurahishwa na taarifa za Simba kubeba ubingwa wa
Mapinduzi na anawapongeza kwa hilo, alisisitiza wana kikosi kizuri, hivyo
wakicheza kwa umoja nyota yao itang’aa zaidi.
“Ninashukuru
nipo na afya njema na ninaendelea na majukumu mengine nje ya soka, asante sana
kwa kunikumbuka.
“Bado
sina timu, tangu tuachane na Simba nilikuwa kwetu mjini Kitwe, lakini jana
(juzi Alhamisi) nimerejea hapa Lusaka. Tunaendelea kufanya mipango ili kupata
klabu ya kufundisha na tukifanikiwa katika hilo basi tutafahamishana.
“Nimesikia
Simba wamepata ubingwa wa Mapinduzi, nimefurahi na ninawapongeza sana kwa hilo.
Wana kikosi kizuri kama wakicheza kwa kujituma zaidi watapata mafanikio
makubwa,” alisema Phiri huku akigoma kuzungumzia lolote kuhusu malipo yake na
Klabu ya Simba.







0 COMMENTS:
Post a Comment