Na
Saleh Ally
STEVE
Mwamwala aliyezaliwa Kyela mkoani Mbeya alipata umaarufu mkubwa ndani na nje ya
Tanzania baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0, mwaka 2012.
Shabiki
huyo wa Yanga wakati huo, alishindwa kujizuia, akamwaga chozi kwa uchungu na
kusababisha wengi kumuonea huruma na umaarufu wake, ukazaliwa.
Hakuwa
tena Steve Mwamwala, badala yake akaanza kujulikana kama Steve Yanga na
umaarufu wake ukapaa haraka mno. Sasa anajulikana kama Steve Azam.
Steve
Azam ni jina jipya baada ya kutangaza kuhamia Azam FC ambao sasa ndiyo mabingwa
wa Ligi Kuu Bara.
Kijana
huyo ameamua kuhamia Azam FC hali ambayo imewaudhi kwa kiasi kikubwa mashabiki
wa Yanga, lakini kubwa zaidi, anasema amepoteza kazi na kuondolewa sehemu
aliyokuwa akiishi.
Hili la kuondokewa kwenye nyumba uliyokuwa ukiishi
lina ukweli?
Ndiyo,
nimefukuzwa kwenye nyumba. Nilikuwa nikiishi Tabata Segerea siku zote lakini
baadaye kigogo mmoja wa Yanga (anamtaja) alinipa kazi na nyumba nzuri. Nilikuwa
nikifanya kwenye Supermarket moja huko Mbezi Beach.
Baada
ya kusikia nimehamia Azam FC, mara moja akanifukuza kazi na kuniondoa kwenye
nyumba. Nimerudi Tabata Segerea.
Vipi kuhusu urafiki wako na mashabiki wa Yanga? Umekuwa mbaya sana kaka, hawataki
kuniona na wamekuwa wakisema vibaya kila wanaponiona. Najiona kama nimetengwa
na siishi na wenzangu.
Kuna taarifa Azam FC, wanakulipa mshahara?
Nani
kasema? Haya ni maneno ya kizushi kabisa. Kweli Azam FC wameniahidi fedha kwa
ajili ya mtaji, lakini hilo lilikuja baada ya mimi mwenye kuhamia kwenye timu
yao, hawakuniomba.
Zaidi
ninachopata kwao ni pale timu inaposafiri, wananijumuisha, naungana nao kwenda
kuwapa nguvu. Hakuna zaidi.
Nasikia umekuwa ukikumbana na vitisho kutoka kwa
mashabiki wa Yanga?
Kweli
kiasi fulani ninaishi kwa hofu. Wengi wao wananiita msaliti, wapo waliokuja
hadi nyumbani na kunitishia lakini sioni kama ni sahihi, maana mimi si adui,
nimeamua kuhama kwa hiyari yangu.
Kweli shabiki anaweza kuhama, hivyo siku moja
tutegemee kukusikia ukiitwa Steve Simba?
Haitatokea
milele. Najua Simba wana watu wengi wenye ushirikiano, wananivitua kwa hilo na
hiyo ni sifa yao nzuri lakini siwezi kuwa Simba, nimehamia Azam baada ya Yanga
na haiwezi kuwa zaidi, siwezi kwenda Simba.
Nini hasa kilichokuondoa Yanga Steve, ni kweli njaa
kama wanavyosema watu wengi?
Njaa
kila mmoja anayo! Hata wewe una njaa Saleh ndiyo maana unaamka asubuhi kuwahi
kazini.
Ila
tatizo kubwa lililonifanya niondoke kulikuwa na kipindi kinaitwa Kwetu House
kilichoendeshwa na Azam TV, nikaenda kushiriki, hapo ndiyo ugomvi ulianza.
Nilikwenda
kama shabiki maarufu wa Yanga. Walikuwepo wa Simba na timu nyingine. Yanga
hawakulifurahia wakawa wananiita msaliti, nikijaribu kufafanya hawakuelewa na
walisisitiza sisi tuna ugomvi na Azam.
Nikawaeleza
mchezo uko Azam TV si Azam FC, lakini wapi. Siku alipokuja Kocha (Marcio)
Maximo nikaenda kumpokea uwanja wa ndege, hapo ndiyo tatizo lilianza.
Mashabiki
kama 50 wa Yanga walinivamia, wakataka kunipiga wakidai mimi ni msaliti.
Nikaokolewa na polisi wa uwanja wa ndege.
Hiyo
tabia ikaendelea, mwisho nikaona hakuna furaha ya ushabiki. Nikaona hata
wachezaji huwa wanahama, nikahamia Azam FC.
Ungeweza kuwa mvumilivu, mwisho wangekuelewa?
Niliishakuwa
mvumilivu sana, kuna wakati tena mashabiki wa Yanga walitaka kunipiga kwa kuwa
niliwazuia wasivunje kamera za Azam TV, nikawaambia hiyo si Azam FC, likawa
kosa.
Mara
mbili kuna viongozi wa Yanga (anawataja) waliwahi kunitukana matusi makubwa.
Sikuelewa kisa, wao ndiyo waliniambia niwatafute, halafu wakanitukana.
Sasa unaishi maisha ya namna gani, unataka uishi
vipi zaidi ya hapo?
Maisha
yangu ni ya kawaida, bado sijapata kazi, naendelea kutafuta. Wale rafiki zangu
niliokuwa nao Yanga, sasa wananipita, hata lifti tu ya gari sipati!
Inaniuma
sana maana Azam FC ni timu kama ilivyo Yanga, sielewi chanzo cha uadui na
michezo haisemi hivyo.
Kuhusu
maisha, nataka niishi maisha mazuri, nioe msichana mzuri kama Wema Sepetu
ambaye ninampenda sana.
Angalia
Idris, leo kama zaidi ya Sh milioni 500. Nilisoma naye huyu Idris, hivyo na
mimi natamani maisha hayo.
Usisahau,
ishu ya kujulikana kama shabiki wa Yanga nilielia, imenipa umaarufu mkubwa
ambao wakati mwingine unanitenda!







0 COMMENTS:
Post a Comment