January 5, 2015


Na Saleh Ally
MWAKA 1972 mchezaji nyota wa Zaire (sasa DR Congo), Tshmeni Bwanga alishika nafasi ya pili ya Mchezaji Bora wa Afrika, mshindi alikuwa Cherif Souleyman wa Guinea.


Mwaka uliofuatia Bwanga akaibuka kuwa Mchezaji Bora Afrika, akifuatiwa na Mwamba Kazadi wa Zaire pia na wote hawa wawili walikuwa wanakipiga katika kikosi cha TP Mazembe.

Mwaka 1974 ambao ulikuwa ni wa tatu, tuzo hiyo ikaenda kwa Paul Moukila wa Congo Brazzaville, nafasi ya pili Lobilo Boba wa Zaire na tatu Hassan Shehata wa Misri ambaye baadaye amekuja kuwa kocha maarufu wa nchi hiyo.

Historia hiyo kwa ufupi, haina utamu wowote kwa Mtanzania kwa kuwa hakuna kinachomgusa zaidi. Ila inaweza kuzua maswali kwamba kumbe DR Congo wamekuwa hadi kwenye nafasi za mchezaji bora Afrika na wamewahi kuitwaa tuzo hiyo.

Hiyo ni sehemu ya ukanda wetu, hata jirani zetu Zambia kupitia Kalusha Bwalya mwaka 1988, halafu 1989, akawa wa tatu mshindi akiwa Joseph-Antoine Bell wa Cameroon.

Tuzo za mchezaji bora mwaka huu, katika majina ya mwisho wale 25 kabla ya fainali yenyewe, Tanzania haina mchezaji hata mmoja.

Lakini kuna listi ya wachezaji 20 ambao watawania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wale wanaocheza ndani ya bara hili, Tanzania haina hata mchezaji mmoja!

Uganda:
Unaweza kusema huko ni kugumu sana, lakini katika wachezaji hao 20 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo kwa wachezaji wanaocheza barani Afrika, jirani zetu Uganda wana wachezaji Yunus Sentam anayekipiga AS Vita ya DR Congo na Geoffrey Massa anayeichezea Pretoria University ya Afrika Kusini.

Katika listi hiyo, DR Congo ina wachezaji wanne, sasa jiulize kwa nini Tanzania tangu enzi hizo haina mchezaji hata mmoja anayewania tuzo hizo?

Kipimo au ubora wa soka ya Tanzania upo wapi? Tutasema, tutaelezwa na kudanganywa hadi lini?

Maswali rahisi, majibu yake ni vigumu kupatikana kwa kuwa wahusika wala hawana habari.

Diamond:
Majibu itakuwa shida, lakini tukumbushane sasa kwamba Tanzania nayo itakuwa sehemu za tuzo hizo zitakazofanyika Januari 8 jijini Lagos, Nigeria.

Kijana huyo anastahili sifa, hakuna ubishi kwamba hajafika hapo kwa nguvu za giza, amejituma, amebuni, amepambana nyumbani, Afrika, Ulaya hadi Amerika. Sasa anakubali.

Hatujui yupi kutoka nchi ipi atashinda katika tuzo hizo za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lakini ubora wa msanii wa Bongo Fleva, Nasib Abdul ‘Diamond’ ndiyo utakaotuwakilisha.

Hakuna ubishi tena, tuzo hizo ni za ubora. Wanaowania lazima wawe bora. Wageni wengi waalikwa ni waliowahi kuwa bora, shujaa wa nchi zao.

Hata watakaotumbuiza, ni wale wanaoonekana kuwa na kiwango bora kinachokubalika Afrika.

Diamond amevuka kwenye suala la rekodi hadi kwenye soka. Huenda Caf wangetamani kumwalika au kumshirikisha hata mmoja katika soka, nani sasa?

Diamond ndiyo mwakilishi na hakuna ubishi anakwenda kwenye tuzo hizo kupitia ubora wake. Tujivunie, ndiyo. Lakini kwa wadau wa soka, lazima tuone aibu, ndiyo!

DR Congo imeanza kufika huko tangu enzi za Zaire, usisahau kwa muziki pia hatuwapati. Zambia pia ambao ni jirani zetu, yaleyale. Leo Uganda nao, wanakwenda huko mara kibao, mwisho utasikia Rwanda, Burundi, sisi tuko hapahapa ‘chai’ nyingi na programu zisizokamilika.

Viongozi wa Yanga, Simba na klabu nyingine acheni blah-blah. Jifunzeni, fanyeni mambo yanayoangalia Bara la Afrika. Kufungana nyie imetosha, kuwa na viongozi wanaotaka sifa pia imetosha. Sasa ni malengo na mafanikio kimataifa.

Timu za Tanzania zikifika mbali kimataifa hasa barani Afrika, hakuna ubishi wachezaji bora wataanza kupatikana.

Kwa wachezaji pia, acheni uvivu, acheni uoga wa kupambana na changamoto. Nendeni mkacheze nje kama wanavyofanya wenzenu wa Uganda, hivyo ndiyo njia rahisi ya kuleta mafanikio nyumbani.

Leo mnajisifia Diamond kufika hapo, lakini naye angekubali kama nyie akabaki kitumbuiza Tandale, Sinza, Mbagala, Ilala na kwingineko, naye asingefika hapo alipo.

Yanga, Simba na wenzao tatizo, wachezaji wao na wameridhika, mashirikisho hasa baba yao, TFF, nao tatizo kubwa!

Hebu hata kidogo muwe mnaumizwa na mafanikio ya wengine. Halafu muweze hata kujiuliza na kubadilisha mambo. Hivi nyie ni watu wa aina gani!!

BAADHI YA WALIOTWAA TUZO ZA MCHEZAJI BORA AFRIKA:
MCHEZAJI                    NAFASI YA       1            2             3
Samuel Eto'o (Cameroon)              4          2         2
George Weah (Liberia)                        3              4              0
Abedi PelĂ© (Ghana)                               3              0              0
Yaya TourĂ© (Ivory Coast)              3              0              0
Didier Drogba (Ivory Coast)              2              4              3
Roger Milla (Cameroon)                 2              2              1
Thomas N'kono (Cameroon)              2              1              1
Nwankwo Kanu       (Nigeria)              2              0              0
El Hadji Diouf (Senega)                       2              0              0
Rashidi Yekini (Nigeria)                       1              1              1
Emmanuel Amuneke (Nigeria)        1              1              0
Tshimen Bwanga (DRC)                     1              1              0
Kalusha Bwalya (Zambia)              1              0              1


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic