Na Saleh Ally
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, amefunga ndoa hivi
karibuni kwao Uganda, hii ni moja ya sehemu muhimu ya kila mmoja duniani.
Baada ya hapo, Okwi alikatiza fungate na kuamua kurejea haraka
jijini Dar es Salaam kwa lengo la kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa.
Taarifa za Okwi angerejea nchini baada ya kukatisha fungate
ziliripotiwa na gazeti hili kwa mara ya kwanza.
Katika mahojiano hayo, Okwi alisema hivi: “Ingawa ndoa ni jambo
muhimu katika maisha yangu, nimeamua kukatisha fungate kwa muda ili nirudi na
kucheza mechi dhidi ya Kagera.
“Nataka nisaidiane na wenzangu maana pointi tatu ni muhimu na Kagera
ni timu ngumu sana. Baada ya hapo, uongozi umekubali utanipa ruhusa nirejee
Uganda kwa ajili ya fungate.”
Alirejea na bahati mbaya lengo lake la kuisaidia Simba kupata pointi
tatu halikufanikiwa. Ikalala bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Simba wakati inasafiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya
Kombe la Mapinduzi, Okwi alifunga safari kurejea Uganda kumalizia hilo fungate.
Uongozi wa Simba ulithibitisha hilo lakini kwa kipindi cha wiki
sasa, inaonekana Okwi amechelewa kufika mazoezini na baadhi ya viongozi wa
Simba wamekuwa wakijikanyaga katika hili.
Nafikiri kuna upungufu sehemu mbili. Wapo viongozi ambao wamekuwa
wazi kwamba Okwi alitakiwa kuwasili nchini leo au kesho kuungana na wenzake kwa
mujibu wa ruhusa aliyopewa.
Lakini viongozi wa Simba ambao wamekuwa wakizungumza kwenye vyombo
vya habari hasa msemaji, Humphrey Nyansio, wamekuwa wakijikanyaga na kushindwa
kuweka wazi lini Okwi alitakiwa kurejea ili kuondoa mkanganyiko.
Hii imechangia kufanya suala la Okwi kuchelewa kurejea kuwa kubwa
sana, lakini hali halisi inaonyesha uongozi unajua ulitoa ruhusa hadi lini.
Wote tunajua Okwi amekuwa msumbufu anapokwenda kwao, tabia ambayo
imekuwa ikiwaudhi watu wengi, mimi mmoja wao.
Lakini safari hii, alimuacha hadi mkewe, siku mbili, tatu baada ya
ndoa akarejea kuichezea Simba, hakusumbua kurudi. Kaondoka kwa ruhusa na
uongozi umethibitisha bado haijaisha, lakini anahukumiwa.
Nia yangu si kumtetea Okwi, nimekuwa wa kwanza kupinga yeye
kuonyesha utovu wa nidhamu na nikasisitiza awaheshimu wachezaji wenzake
wazalendo, aache nyodo na kama mkongwe awe mfano.
Katika hili la kuchelewa kurejea kwenye michuano ya Mapinduzi, basi
tunapaswa kukubali kuwa mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.
Kama angekuwa amekosea, viongozi wangesema. Kukaa kwao kimya maana
yake wanajua kwamba walimpa ruhusa aende na wanajua atarudi lini.
Kama nilivyoeleza, shida yao wameshindwa kuliweka suala hilo wazi,
kama vile wanahofia kitu. Ukweli wanajua siku ya Okwi.
Sasa nafikiri busara itakuwa ni kuacha Okwi achelewe kwanza ndiyo
tunaweza kuanza kumjadili. Kumhukumu sasa wakati uongozi unajua umetoa ruhusa
hadi lini ni kulazimisha kosa kupitia rekodi zake za nyuma.
Kwamba amekuwa akichelewa kila anapokwenda nyumbani, kweli.
Tukubali, sasa hajachelewa na hatuna haja ya kulazimisha kuonyesha amechelewa.
Angalau tuonyeshe kukubali vichache vyake hata kama amekuwa akikosea
sana. Kitendo cha kuamua kurejea kuja kuichezea Simba katika mechi dhidi ya
Kagera pia kilikuwa kina uzalendo au mapenzi ndani yake.
Najua hakuna aliyekuwa amempongeza, mimi nampongeza na kumuasa kuna
kila sababu ya kubadilika zaidi ya hapo na ikiwezekana awe mfano wa kuigwa si
kwa uwezo uwanjani pekee, lakini hata katika maisha ya kila siku kwa kuwa sasa
si kijana Okwi tu, badala yake ni Mr Okwi, maana tayari ana familia na ndiyo
imeanza.







0 COMMENTS:
Post a Comment