![]() |
| AJIBU (ALIYEPIGA MAGOTI) AKISHANGILIA NA WENZAKE BAADA YA KUFUNGA MOJA YA MABAO... |
JUZI Jumatano usiku, Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi
ya Taifa Jang’ombe na kutinga kwa kishindo katika hatua ya Nusu Fainali ya
Kombe la Mapinduzi inayoendelea kisiwani Zanzibar.
Mchezaji
chipukizi katika kikosi cha Simba, Ibrahim Ajibu aliyeingia katika kipindi cha
pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma na kutupia mabao matatu ‘hat trick’ kisha
Shaban Kisiga kufunga moja, amekuwa gumzo kila kona.
Ajibu
ambaye mashabiki wa Simba wanaamini ndiye Haruna Moshi ‘Boban’ mpya kikosini
hapo, alionyesha kiwango kikubwa katika mechi hiyo kiasi cha kuwatisha
wapinzani wanajiandaa kukumbana na Simba.
Mchezaji
huyo mwenye majina mengi ya utani yakiwemo Ibracadabra, Mido na Milito,
amezungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, jana Alhamisi, akatiririka:
Ulijisikiaje
kufunga hat trick?
Nilijisikia
furaha mno kuona naingia uwanjani timu ikiwa haina matokeo lakini nakwenda kuwa
chachu ya ushindi, ni jambo zuri zaidi kwangu kwenye historia ya maisha yangu
ya mpira.
Kocha
alikwambia nini ulipokuwa unaingia?
Wala
hakuniambia maneno mengi, alitunyanyua tu kwenye benchi mimi na Simon
(Sserunkuma) akatuambia kuwa mechi imeshakuwa ngumu na ninyi ndiyo tegemeo
langu la mwisho kwa ajili ya kubadili matokeo, basi tukaingia na Mungu
akasaidia kweli tukabadili matokeo.
Ukiwa
uwanjani unajiamini sana, siri ni nini?
Yaani
hakuna kitu kingine zaidi ya kujiamini, ndiyo maana huwa nafanikiwa mara
nyingi.
Nafasi
ipi unamudu zaidi uwanjani?
Nashukuru
nimejaaliwa uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo mshambuliaji kuanzia pembeni
mpaka katikati lakini nafurahi zaidi nikicheza namba 10.
Vipi
kuhusu ushindani wa namba?
Ushindani
upo lakini naamini nitacheza kwenye kikosi cha kwanza muda si mrefu kwa kuwa
kocha aliyekuja sasa (Goran Kopunovic) amesema anampanga mtu kutokana na bidii
yake.
Nani
alikuleta Simba?
Mara
ya kwanza bro Patrick (Rweyemamu, Meneja wa Simba B) ndiye alinikaribisha
nijiunge na Simba B kama miaka minne hivi iliyopita baada ya kuniona kwenye
moja ya ‘game’ zangu za uswahilini. Baadaye niliondoka na hivi karibuni
nikaitwa tena.
Nani
aligundua kipaji chako?
Namshukuru
sana mama yangu, kwani ndiye aliyekuwa akinishikilia sana na kunipa sapoti
katika ishu zangu za mpira, yupo Uarabuni lakini amekuwa anikiunga mkono kwa
kila nachokifanya.
Unafikiri
Kopunovic atarejesha heshima ya Simba?
Namwamini
sana huyu mwalimu, ana falsafa zake ambazo naamini zitasaidia sana kuijenga
timu na kukaa kwenye mstari.
Taji
la Kombe la Mapinduzi litatua wapi?
Nina
imani kubwa tutalibeba kombe kwa sababu katika timu zilizobaki, zote tunaweza
kupambana nazo na pengine hata kuzishinda na kutimiza azma yetu.
Vipi
kuhusu ufungaji bora?
Ni
kweli Msuva (Simon wa Yanga) ana mabao manne, yupo juu yangu kwa bao moja
lakini kama nitapata nafasi katika mechi zilizobaki, nitajitahidi kufunga
kadiri ya uwezo wangu kisha mwisho wa mashindano tutajua nani kafanikiwa.
Ulianzia
wapi soka?
Nilianzia
soka la ushindani katika ile timu ya Boom FC ya Ilala kwenye Ligi Daraja la
Pili na la Kwanza, nikaenda Simba B baadaye nikatimkia Mwadui ya Shinyanga na
msimu huu ndiyo nimetua Simba.
Ndoto
zako zipoje?
Ningependa
siku moja niwe mchezaji wa soka la kulipwa nje ya nchi.








0 COMMENTS:
Post a Comment