Timu ya Taifa
ya Tanzania ya mpira wa ufukweni (beach soccer) imepangiwa kucheza na Kenya
katika raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa ajili ya fainali za Afrika za
michuano hiyo zitakazofanyika Aprili mwaka huu nchini Shelisheli.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Beach Soccer, Ahmed Idd Mgoyi amesema jijini Dar es Salaam, leo kuwa
Tanzania itaanzia ugenini ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13
na 15 mwaka huu nchini Kenya.
Mechi ya
marudiano itafanyikaa nchini kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu. Iwapo timu ya
Tanzania itasonga mbele, katika raundi ya pili itacheza na Misri ikianzia
nyumbani kati ya Machi 13 na 15 mwaka huu.
Mgoyi alisema
maandalizi ya Tanzania kushiriki kwenye mashindano hayo yameanza ambapo timu ya
Tanzania Bara itacheza na Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata kikosi
kimoja kitakachoingia kwenye michuano hiyo ya Afrika.
Alisema benchi
za ufundi la timu ya Tanzania litaongozwa na John Mwansasu wakati Msaidizi wake
ni Ali Shariff 'Adolf' kutoka Zanzibar, na Meneja wa timu hiyo ni George Lucas.
Wote hao walishiriki kwenye kozi ya ukocha wa beach soccer iliyoendeshwa mwaka
jana nchini na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kocha Mwansasu
atatangaza timu ya Tanzania Bara, Januari 19 mwaka huu, na mazoezi ya pamoja na
timu ya Zanzibar yatafanyika Januari 24 na 25 mwaka huu.
Wachezaji wa
timu ya Tanzania Bara watatokana na michuano ya beach soccer iliyofanyika mwaka
jana ikishirikisha timu za vyuo vya elimu ya juu vya Mkoa wa Dar es Salaam.








0 COMMENTS:
Post a Comment