MAPEMA mwezi huu waamuzi mbalimbali katika
mechi za Ligi Kuu Daraja la Kwanza walikutana na dhoruba kali ya kupigwa kama
wezi.
Kupitia gazeti hili tuliona mwamuzi
aliyechezesha mechi ya Toto African dhidi ya Polisi Dodoma akikimbizwa kama
kibaka huku akipigwa na mchezaji ambaye sura yake ilionekana dhahiri ni nani.
Hii ilitokea kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Siku chache badaye kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba tena, wachezaji wa Polisi Tabora nao waliwapiga waamuzi huku
wakiwakimbiza kama vibaka pia.
Kwa kuwa hali hiyo ilionyesha mashabiki,
walifikia uamuzi wa kuteremka jukwaani na kuanza kutaka kupambana na wachezaji
wa Polisi Tabora lakini askari Polisi wakapoza vurugu hizo na mwisho
wakamrudisha mwamuzi uwanjani chini ili amalize mpira.
Usisahau mara ya kwanza, yule mchezaji wa
Polisi Dodoma alimkimbiza mwamuzi hadi jukwaani naye akakutana na kipigo kutoka
kwa mashabiki.
Kila kitu kilikuwa wazi, tena nyongeza
vurugu kama hizo zilitokea kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma na mwisho TFF
ikatangaza kuufungia uwanja huo ambako wachezaji wa Mwadui FC, Kocha wao,
Jamhuri Kihwelo Julio na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga
(Shirefa), Kangi Lugola nao walipogwa kama wezi.
Ajabu TFF imeanza kulishughulikia suala hilo
huku wakionyesha wazi kwamba wale wachezaji waliowapiga waamuzi huku
wakiwakimbiza si wote walioshitakiwa.
Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd Hussein,
Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT na Nassib Lugusha wa Polisi
Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi na
kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani.
Lakini wengine waliofikishwa kwenye kamati
ya nidhamu ni watunza vifaa wa Polisi Mara, Rhino na JKT Oljoro. Kocha wa
Polisi Tabora, Kim Christopher analalamikiwa kumtolea mwamuzi lugha chafu.
Sasa swali langu linafuatia hapo, wako wapi
wale wachezaji ambaow anaonekana wazi wakiwakimbiza waamuzi huku
wakiwashambulia kwa ngumi na mateke.
Angalia mchezaji wa Polisi Dodoma,
alimkimbiza mwamuzi ambaye alianza kumpiga uwanjani, akatoka naye hadi jukwaani
ambako alipigwa na mashabiki. Hali kadhalika, wachezaji wa Polisi Tabora ambao
walimpiga mwamuzi kama kibaka.
Picha zinaonyesha wakiwa wamempiga mateke na
kuna picha inaonyesha mchezaji mmoja wa Polisi Tabora akiwa amempiga ngumi
mwamuzi wa akiba!
Jamani, kama kweli waliofanya vile wameachiwa tu na TFF
inaona ni sawa, basi hapa tutaanza kujenga hisia timu za majeshi zinaogopwa
hadi na shirikisho hilo.
Jiulize, vipi mchezaji anayempiga mwamuzi kama kibaka,
haladu anaonekana kabisa kwamba ni yeye na adhabu haitoki. Tunautengeneza vipi
mpira wetu.
Inawezekana kabisa jambo hilo limechukuliwa kwa uzito wa
chini kabisa, kitu ambacho kinadhibitisha hakuna anayewajali waamuzi.
Sitaki kuwatetea waamuzi kwamba ni watu safi kuliko
wengine wote. Kuna matukio mengi sana yanathibitisha wanapokea rushwa ingawa
wanatumia nguzo ya usiri kama sehemu ya kufunika kombe.
Lakini bado hatuwezi kuunga mkono wapigwe kwa wezi hali
ambayo inaleta taswira tofauti inayolenga kuuporomosha mpira wa Tanzania na
kuuonyesha kama ni mchezo wa wahuni fulani.
Wakati mwingine najiuliza au TFF inaona haya kwa kuwa
picha zimetoka kwenye gazeti hivyo haiwezi kuchukua uamuzi wowote kwa kuwa
itaonekana “imefanya kazi kupitia gazeti au blogu?”
Inapaswa kujifunza, gazeti katika kamati ya nidhamu
linaweza kutumika kama ushahidi. Raha zaidi ni picha na si maandishi na huenda
gazeti linaweza kuaminika zaidi hata kuliko ripoti ya kamisaa na hasa picha
zikitumika.
Kuna kila sababu ya wachezaji wa Polisi Dodoma na Tabora
waliowapiga kuadhibiwa. Pia wenzao wa Polisi Mara na uongozi wao. Mkiwaacha hao
maana yake mnatoa ruhusa na wengine wafanye.
0 COMMENTS:
Post a Comment