Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa,
ametoroka nchini na kukimbilia kusikojulikana huku viongozi wake wakijua kuwa
amekwenda Tanga kwa ajili ya msiba wa mamamkwe wake.
Ngassa hajaonekana Yanga tangu Jumanne ya wiki
iliyopita. Aliwaaga viongozi wa klabu hiyo kuwa anakwenda Tanga kuhudhuria
msiba lakini taarifa zinadai ametoroka nchini.
Chanzo chetu cha habari kimesema winga huyo
ameonekana akipanda ndege kuelekea Afrika Kusini.
Bado haijawekwa wazi kuwa amekwenda kufanya
nini lakini inaaminika amekwenda katika Klabu ya Free State ya Afrika Kusini
kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Championi Jumatatu ilipomuuliza katibu wa
klabu hiyo, Dk Jonas Tiboroha, alisema Ngassa aliwaaga kuwa anakwenda msibani
Tanga ambapo alifiwa na mamamkwe na si vinginevyo.
“Sisi alituaga kuwa alipatwa na matatizo ya
kifamilia, kwamba alifiwa na aliondokewa na mamamkwe wake, kama ni hizo habari
nyingine binafsi sina,” alisema Dk Tiboroha.
Chanzo cha habari chetu kilikwenda mbali na
kusema kuwa, uongozi hautaki kuliweka wazi suala hilo ingawa wameandaa adhabu
ya kutosha kama fundisho kwa wachezaji wengine kwa ukosefu wa maadili ya
kikazi.
“Kuna watu walimuona akipanda ndege ya Sauz,
kwa hiyo viongozi wanasema bado wanalichunguza kwa umakini ili wajiridhishe
kuhusu safari yake na iwapo itabainika kweli alikuwa Sauz, kitakachomkuta ni siri yao, ila ni adhabu ambayo
itakuwa fundisho kwa wenzake wanaofanya mambo ya Kiswahili,” kilisema chanzo
chetu.
Ngassa alipotafutwa kwa
simu yake ya mkononi ambayo amekuwa akiitumia Tanzania, hakuweza kupatikana kwa
siku nzima ya jana, hali inayoonyesha kuwa hayupo nchini.
Kwa siku za hivi karibuni, Ngassa amekuwa
katika mgogoro wa chinichini ya Yanga, hasa kutokana na uongozi wa klabu hiyo
kukiuka makubaliano ya kumlipia kiasi cha Sh milioni 45 anachodaiwa na Simba
kutokana na adhabu aliyopewa na TFF kwa kusaini klabu mbili mwaka 2013.
Yanga ilikuwa imekubaliana na kiungo huyo
kwamba itamlipia nusu ya deni wakati alipokuwa akisaini kuichezea Yanga mwaka
2013 na kiasi kingine watakuwa wakimkata kidogokidogo kwenye mshahara lakini
badala ya kumkata Sh 500,000 kama makubaliano yalivyo, wamekuwa wakimkata Sh
1,000,000 hali inayodaiwa kumuondolea morali na kumfanya acheze chini ya
kiwango.
0 COMMENTS:
Post a Comment