Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,
Zacharia Hans Poppe amefunguka kuhusiana na suala la kiongozi aliyetajwa kuwa
anamshinikiza kocha katika upangaji wa timu.
Siku nne zilizopita, SALEHJEMBE iliandika
kuhusiana na kuwepo kwa taarifa za uhakika kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Goran
Kopunovic alimtaja mtu ambaye amekuwa akihusika na kumshinikiza kocha huyo
katika upangaji hadi fomesheni.
Leo mchana, SALEHJEMBE, ikatupia makala
iliyokuwa ikieleza ni jambo jema kwa uongozi wa Simba kumuweka kiongozi huyo
hadharani ili kuondokana na ile kashfa na mambo mengi yanayohusu kuwapangia
waamuzi listi au kushinikiza wachezaji fulani wacheze.
Akizungumza kutoka Dubai, Falme za Kiarabu,
Hans Poppe alisema ameamua kutoa ufafanuzi huo baada ya kusoma makala
iliyoandikwa na blogu hii.
“Unajua hili suala haliwekwi vizuri huenda
kwa kuwa ni taarifa za ndani. Lakini ukweli kocha alimtaja huyo mtu na kusema
kuna wakati aliwahi kutoa ushauri naye akaukataa.
“Mimi ndiye nilimuuliza kocha kuhusiana na
kwamba je, amekuwa akiingiliwa kwa lolote katika suala la upangaji wake wa
timu, akasema hapana.
“Lakini akamtaja huyo kiongozi na kusema
kuna wakati akiwahi kutoa ushauri wa kuchezesha straika mmoja juu badala ya
wawili.
“Kocha akamuambia hilo ni suala la baadaye
baada ya wachezaji na kikosi kuzoeana na baada ya hapo anaweza kuhamia kwenye
aina nyingine ya mifumo.
“Hivyo haikuwa kumpangia kwa kuwa
hakumlazimisha, ndiyo maana kocha alikuwa na uhuru wa kukataa.
“Kama angekuwa anamlazimisha, maana yake
angemlazimisha yeye kama kiongozi kwamba ni lazima amtumie mchezaji fulani au
atumie mfumo fulani na kocha asingeruhusiwa kukataa.
“Nimetaka kuweka hili suala sawa namna hii
ili watu waelewe. Kuna watu wengi wamekuwa wakimpigia kocha na kutoa maoni yao,
amesema wengine ni wanachama, mashabiki na hata waandishi.
“Ingawa amekuwa hana uhakika ya wao ni akina
nani hasa na wamepata vipi namba yake. Hivyo hili suala liko namna hii,”
alifafanua Hans Poppe.







0 COMMENTS:
Post a Comment