Na Saleh Ally
AWALI nilidhani ni
mashabiki wa Arsenal wa nyumbani Tanzania pekee ambao wamekuwa wakimlalamikia
Kocha Arsene Wenger kuwa ni tatizo hasa kila Arsenal inapopoteza mchezo.
Nikiwa katika mazungumzo ya
kawaida na rafiki yangu anayeishi London, tena shabiki wa kutupwa wa Arsenal,
naye alianza kuangusha lawama kwa Wenger kwamba ndiye anawakwamisha hasa baada
ya kufungwa mabao 3-1 na Monaco.
Mtu mwingine ambaye ni mchambuzi wa michezo nchini Msumbiji
alikuwa akinisimulia maendeleo ya soka la Ureno ambako alifanya ziara hivi
karibuni. Hakuacha kumponda Wenger pia, kuwa ni ‘kirusi’ ndani ya Arsenal!
Watu hawa wawili
walinirudisha nyuma na kuanza kutafakari kwamba huenda mashabiki wa Arsenal
ndiyo wanaoongoza kuliko wote kwa jazba. Au wao wanaongoza kwa kuwa na lawama,
bila ya kufuatilia.
Watu wawili niliozungumza
nao katika mazingira tofauti, wote ni wataalamu katika masuala ya michezo, kwa
nini hawaelewi? Kama wao hawaelewi, vipi kwa shabiki wa kawaida?
Mechi 10:
Nikaamua kurejea kwenye
takwimu za mechi 10 za Arsenal ikiwemo hiyo dhidi ya Monaco. Hesabu zikazidi
kunishangaza zaidi kuhusiana na Wenger, kwamba wanamuonea, watamuua huyu mzee.
Kuanzia Januari 4, hadi
Februari 25 mwaka huu walipocheza mechi na Monaco, Arsenal walikuwa wamecheza
mechi kumi mfululizo.
Walicheza mechi hizo kumi
za michuano ya Kombe la FA, Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa ndani ya siku
53, tena wakiwa wamepoteza michezo miwili tu.
Mechi ya kwanza walipoteza
Februari 4 wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa White Lane, London baada ya kufungwa
mabao 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur kabla ya kuchapwa na Monaco kwa mabao 3-1 wakiwa kwao
Emirates.
Ukiachana na hapo, Arsenal
imecheza mechi sita za nyumbani na kushinda tano, huku ikipiga nne za ugenini
na kushinda tatu.
Ukimya:
Wakati Arsenal ikiendelea
kushinda mechi mfululizo, hakuna shabiki aliyekuwa akilalamika zaidi ya kusifia
wachezaji walivyokuwa wakifanya vizuri.
Mfano, wengi walisifia
kurejea kwa Mesut Ozil, kwamba sasa atakuwa tishio na alivyokuwa anakwenda
ilionekana wazi hakuna wa kumzuia.
Mwingine ni Santi Cazorla,
yuko vizuri na hilo ni kweli. Wengi walimwaga sifa kutokana na uwezo ambao
amekuwa akiuonyesha katika mechi za hivi karibuni.
Ingawa kumekuwa na hofu
kwamba, Alexis Sanchez amepunguza kasi lakini kurejea kwa Theo Walcott pia
kumeamsha matumaini kwamba Arsenal sasa ina kikosi kipana. Usisahau Olivier
Giroud amekuwa akiwasha moto ile mbaya.
Utagundua kitu hapa, hakuna
aliyekuwa akimzungumzia Wenger kwa ubora wa upangaji timu au vyovyote vile.
Lakini kupoteza mechi mbili ndani ya 10, limekuwa tatizo kubwa sana! Lawama
zote kwake, mtamuua.
Ligi kuu:
Rekodi ya mechi sita
zilizopita kwenye Ligi Kuu England zinaoneysha Arsenal imeshinda tano na
kupoteza moja na iko katika nafasi ya tatu.
Ukichukua timu tano za juu katika
msimamo, zinaonyesha Arsenal ndiyo yenye rekodi bora zaidi angalau vinara
Chelsea ambao katika mechi sita wana sare mbili. Wengine wote kama Man City,
Man United na Southampton, hawaifikii Arsenal kwa kuwa wamepoteza zaidi au
lundo la sare.
Dhidi ya Monaco:
Mashabiki wa Arsenal hawana
lolote la kumlaumu Wenger. Hata wakati wanakwenda katika mechi dhidi ya Monaco
walikuwa na matumaini makubwa kwa kuwa uchezaji wa timu katika mechi za nyuma
ulikuwa bora.
Kufeli kwa kikosi cha siku
hiyo kikiwa na Cazorla, Sanchez, Ozil, Giroud, Danny Welbeck na wengine wote
waliokuwa wanalaumiwa, tatizo ni kwa Wenger pia? Alikosea nini hasa?
Mchezo wa soka una mambo
mengi, wakati mwingine mchezo hukataa kwa mchezaji mmoja, lakini mchezo unaweza
kukataa kwa timu kabisa.
Bado rekodi zinailinda
Arsenal, kwani ndani ya mechi 10 za nyumbani na ugenini, imepoteza mbili tu.
Imefunga mabao 23 na kufungwa manane tu.
Lakini bado mashabiki wa
Arsenal ‘wamekalili’ na wanaamini Wenger ni tatizo, tena wanasema bila ya
kufanya uchunguzi kwanza. Msisahau hata wakati Sir Alex Ferguson akiwa
Manchester United wengi walisema ni tatizo, aondoke. Leo kila mmoja anamlilia.
Mtamkumbuka huyu Wenger.
MICHEZO:
Jan 4
Arsenal 2 – 0 Hull City
Jan 11
Arsenal 3 – 0 Stoke City
Jan 18
Man City 0 – 2 Arsenal
Jan 25
Brighton 2 – 3 Arsenal
Feb Mosi
Arsenal 5 – 0 Aston Villa
Feb 7
Tottenham 2 – 1 Arsenal
Feb 10
Arsenal 2 – 1 Leicester
City
Feb 15
Arsenal 2 – 0 Middlesbrough
Feb 21
Crystal Palace 1 – 2
Arsenal
Feb 25
Arsenal 1 – 3 Monaco
TAKWIMU:
Mechi 10
Wameshinda 8
Wamefungwa 2
MABAO:
Wamefunga 23
Wamefungwa 8
Ndani ya siku 53, wamecheza
mechi 10 ambazo ni dakika 900.
0 COMMENTS:
Post a Comment