Baraka
Kizuguto umepata nafasi ya kuwa Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuondoka Yanga.
Nafasi
uliyoipata, haiwezi kuwa bahati nasibu kwa kuwa tumeelezwa kuna wengine
takribani kumi walijitokeza kuiwania.
TFF
wamekupa nafasi hiyo kwa kuwa wanatambua una taaluma mbili, kwanza uandishi wa
habari na pili IT (teknolijia ya mitandao).
Kwamba
unaweza kubuni au kutengeneza tovuti za aina mbali, lakini unaweza kuendesha
tovuti. Pia ni mmoja wa Watanzania wachache wanaoweza kufanya kazi wakati wa
dirisha la usajili kupitia utaalamu wa TMS.
Katika
hili narudia kauli yangu kwamba haukubahatisha, badala yake vitu ulivyonavyo
vimekupa nafasi hiyo.
Kabla
haujaondoka Yanga ulikuwa na malumbano mara kadhaa na waandishi wa habari, mimi
mmoja wapo.
Lakini
tuliwahi kukutana, nilikueleza malalamiko yangu na vitu ambavyo sikupendezewa,
mwisho tulifikia mwafaka na tukashirikiana kikazi.
Sikuwahi
kushirikiana nawe kikazi tokea umeondoka Yanga, hivyo nakukaribisha tena
nikiamini kupitia Yanga utakuwa umejifunza mengi ingawa utakuwa una changamoto
kupitia Boniface Wambura.
Wambura ni kati ya waandishi wakongwe wa michezo nchini, naamini utendaji wake ulikuwa wa kiwango cha juu na utalazimika kujifunza zaidi.
Wako
wanaotamani ukosee na huenda wakakaa mkao wa kula wakisubiri lini utateleza.
Lakini kama unataka kujifunza, haupaswi kuwa na hofu na unaweza kutenda kwa
kuangalia mazuri na mabaya.
Maadui
hawawezi kukosekana, hauwezi kujua nafasi uliyoitaka, huenda wako walioitaka au
walitaka wapate rafiki zao wa karibu, hivyo wanaweza wasipendezewe.
Ushauri
wangu, haupaswi “kutanua masikio” na kuyafanya yasikilize hata visivyokuwa vya
msingi badala yako majibu yawe kwa vitendo.
Kwa
kuwa unafanya kwenye taasisi ya umma, pia usiwe mbishi kukosolewa inapotokea na
kikubwa ni kuwa mtu unayeamini, kila unapokosea unapata nafasi ya kujua jambo
jipya na kujirekebisha, maana yake faida ni mara mbili.
Kawaida
yangu sijawahi kukata tamaa au kukatishwa tamaa na wale wanaosema wakiamini
kusema ni kunichanganya.
Kila
mtu ana aina yake, wewe unaweza kuwa tofauti na kuumizwa. Lakini kazi yako
ndiyo Watanzania wanaoisubiri na huenda wale wasiofurahia hatua zako wakakosa
la msingi la kuzungumza kama utakuwa mchapakazi.
Kubaki
ukishindana nao ni kupoteza muda, kulazimisha kujibizana nao ni kupunguza kasi
ya utendaji wako.
Kwangu
nikuahidi ukiwa tayari tutashirikiana, ukiwa hauelewi nitakukosoa lakini
nikuhakikishie nakuombea ufanikiwe kwa kuwa utendaji wako ukiwa bora,
tutaendelea kuusaidia mpira wetu wa Tanzania na hilo ndilo lengo namba moja.
Kumlazimisha
punda akimbie kama farasi, ni kumtafutia kifo. Kuyalazimisha masikio yako
yasikie yasiyo na maana ni kupoteza wakati, piga kazi tushirikiane kuusongesha
mpira wetu na kuthibitisha kwamba taaluma ya habari ni sehemu ya mchango.
Ahadi yangu ni kukuunga mkono bila ya woga, kukosoa inabidi bila ya kuyumba na kuungana na wewe panapokuwa panahitaji utaifa.
Karibu
tuungane mkono, karibu tena tukosoane kwa ajili ya kuusaidia mpira.








0 COMMENTS:
Post a Comment