Kocha Goran Kopunovic amefanya mapinduzi kwenye uongozi wa Simba baada ya kumtaja mmoja wa viongozi ambaye amekuwa akimpangia listi na wakati mwingine kumuelekeza timu icheze vipi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza Kopunovic amemtaja kiongozi huyo mbele ya viongozi wengine.
"Unajua viongozi tokea tumeingia madarakani tumekuwa tukituhumiwa suala la kupanga listi. Lakini sisi hatujawahi kufanya hivyo, ndiyo maana tumekuwa tukishangaa.
"Sasa kocha huyu ameonekana kuwa mkweli na mwisho amesema ukweli. Yule kiongozi mwenzetu tukamhoji kuhusiana na hilo, akakataa katakata.
"Tulichofanya tulimuita kocha, naye akamueleza mbele yetu na mifano yote na hata mwenyewe akashindwa kujitetea zaidi," kilieleza chanzo cha uhakika.
Kiongozi huyo ameelezwa kuwa tatizo kutokana na ubishi na ubinafsi, hali iliyosababisha wezake kutokuwa wakimwani.
Mara kadhaa, viongozi Simba wamekuwa wakituhumiwa kuwapangia listi makocha wao, lakini wamekuwa wakikanusha jambo hilo.
Huenda kwa kuwa wamefanikiwa kumpata mhusika, inaweza kuwasaidia kulimaliza tatizo hilo ambalo walivikwa wote wakionekana ni tatizo lao wote.







0 COMMENTS:
Post a Comment