LONDON, England
UTAMU wa soka la Ulaya
utaendelea wikiendi hii. Vita ya kusaka ubingwa wa England nayo itazidi kupamba
moto katika mechi za leo na kesho, lakini kubwa zaidi linalozungumzwa kitaa ni ‘derby’
(mechi zinazohusisha timu zinazotoka mji mmoja) mbili kubwa nchini England.
Derby ya kwanza inatarajiwa
kuchezwa kwenye Uwanja wa White Hart Lane ambayo itazikutanisha timu
zinazotokea katika Jiji la London, yaani Tottenham Hotspur dhidi ya Arsenal
katika mtanange wa kukata na shoka utakaochezwa kuanzia saa 9:45 alasiri.
Lakini baadaye saa 2:30
usiku, kutakuwa na derby nyingine itakayozikutanisha timu zinazotokea jijini
Liverpool, yaani Everton na Liverpool FC ambazo zitapambana vikali kwenye
Uwanja wa Goodison Park.
Tottenham vs Arsenal
Vita hii inasubiriwa kwa
hamu kubwa na mashabiki wa soka sehemu mbalimbali duniani. Mechi itachezeshwa
na mwamuzi mkongwe, Martin Atkinson, raia wa England.
Utamu wa mechi hii
unatokana na timu zote kuwa kwenye kiwango bora katika mechi zake za hivi
karibuni. Katika michezo yao mitano iliyopita, Tottenham wameshinda mitatu,
wametoa sare mmoja na kupoteza mmoja, wakati Arsenal wenyewe wameshinda michezo
yao yote mitano iliyopita.
Katika michezo yao mitano
iliyopita waliyokutana, Arsenal imeshinda mara tatu, wakati Spurs imeshinda
mara moja tu huku zikitoka sare mara moja.
Hata hivyo, pamoja na
Arsenal kushinda mara nyingi dhidi ya wapinzani wao hao katika siku za hivi
karibuni, bado mpambano unatarajiwa kutotabirika kutokana na kiwango cha sasa
cha Spurs ambayo inawategemea zaidi washambuliaji wake Harry Kane na Christian
Eriksen walio kwenye ‘fomu’ kwa sasa.
Supastaa wa Arsenal, Mchile,
Alexis Sanchez, anatarajiwa kuukosa mchezo huo wa leo kutokana na kuendelea
kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja yaliyomuweka nje ya uwanja katika
ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Aston Villa wiki iliyopita, lakini kocha Arsene
Wenger atashusha pumzi kufuatia kurejea kwa mpachika mabao wake, Danny Welbeck.
Timu zote hizi, zipo katika
mapambano ya kuhakikisha zinakuwemo ndani ya nne bora ili zipate nafasi ya
kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kama Arsenal iliyo katika nafasi
ya tano ikishinda kwenye mtanange huu, itakuwa imeingia hadi kwenye mbio za
kuwania ubingwa wa England kwa kuwa itakuwa imebakiza pointi nane tu iwafikie
vinara Chelsea ambao baadaye watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Aston Villa.
Lakini Spurs ikifungwa itakuwa inazidi kujiweka pabaya katika vita ya kuingia ‘top
4’.
Kama Spurs iliyo katika
nafasi ya sita ikishinda mchezo huo, itaipiku Arsenal kwenye nafasi ya tano na
inaweza ikaingia moja kwa moja ndani ya nne bora na kusubiri matokeo ya
Southampton ambayo itakuwa mgeni wa QPR baadaye jioni.
Liverpool vs Everton:
Huu ni mtanange mwingine
ambao umeshaanza kuwa gumzo mjini. Liverpool iliyo nafasi ya saba, iliuanza
msimu huu kwa kusuasua kutokana na kuonekana kummisi mpachika mabao wao
aliyeondoka, Luis Suarez, lakini sasa inaonekana kuanza kuimarika, hasa
kutokana na ubora unaoonyeshwa na viungo wawili wa timu hiyo, Raheem Sterling
na Philippe Coutinho.
Kwa upande wa Everton
wanaonekana kutokuwa sawa msimu huu, kwani wameshindwa kuonyesha makali yao ya
msimu uliopita ambapo walikuwa wanapigania kuingia kwenye ‘top 4’.
Everton wapo katika nafasi ya
12 na wanatakiwa washinde ili kujiondoka kwenye hatari yoyote ya kushuka daraja
na kujiongezea matumaini ya kutafuta nafasi ndogo waliyonayo ya kushiriki
michuano ya Ligi ya Europa, lakini Liverpool bado wanapambana kuingia ndani ya
nne bora.
Pambano hili litachezeshwa na
mwamuzi Muingereza, Antony Taylor. Katika mechi zake tano zilizopita, Liverpool
imeshinda mbili, imetoa sare mbili na kupoteza moja, wakati Everton wameshinda
mechi moja tu kati ya michezo yao mitano iliyopita huku mingine wakitoa sare.
Takwimu zinaonyesha kuwa,
kwenye mechi tano zilizopita baina ya timu hizo, Liverpool imeshinda mara moja
huku matokeo mengine yakibaki kuwa ni sare. Ngoma itakuwa pevu leo na lolote
linaweza kutokea.









0 COMMENTS:
Post a Comment