Giza jijini Milan….
Na Saleh Ally
KILA timu ya Ligi Kuu
Italia ‘Serie A’ imebakiza mechi 16 kuhitimisha msimu wa 2014-15 na pia kupata
uhakika nani atakuwa bingwa tena.
Juventus kutoka Turin ambayo
safu yake ya ushambuliaji inaongozwa na Muargentina, Carlos Tevez inaendelea
kukimbiza ile mbaya kwa kuwa na pointi 53 kileleni.
Timu mbili pekee za AS Roma
yenye pointi 46 na Napoli yenye pointi 42 ndizo zinazoonekana kuifukuza kwa
kasi timu hiyo ya Turin kuuwania ubingwa huo wa Italia.
Kazi si rahisi, Juventus
inatakiwa kushinda wastani wa mechi 10 kati ya hizo 16 ili kujihakikishia
nafasi ya kuwa mabingwa tena.
Wakati Juventus ikiwa
inapambana kuendeleza heshima ya ubingwa, mambo katika Jiji la Milan
yanaonekana kuwa hovyo kabisa na unaweza kuyafananisha na kiza au giza.
Miaka minne iliyopita,
kawaida timu tatu za AC Milan, Juventus na Inter Milan ndizo zilizokuwa
zinafukuzana kwa kasi kileleni hasa inapofikia hatua kama hii.
Leo, baada ya mechi 22, AC
Milan na Inter Milan kutoka katika jiji hilo la kimahaba wana pointi 29 tu kila
upande, tena zikiwa katika nafasi ya 10 na 11!
Kila timu kati ya hizo
mbili imewahi kuwa bingwa wa Ulaya kwa nyakati tofauti. Ndiyo baadhi ya timu
chache zilizobeba heshima ya soka la Italia.
Kama unakumbuka zinatumia
uwanja mmoja, lakini unakuwa na majina mawili, San Siro na Giuseppe Meazza,
kulingana na unatumiwa na timu ipi. Ndiyo timu zenye upinzani mkali Ulaya
lakini zinatumia uwanja mmoja kama ilivyo kwa Simba na Yanga, hapa nchini.
Lakini sasa zinaonekana kupotea
na hata kufikia hatua ya kutia hofu kutokana na mwenendo wake wa kupapasa
gizani ili kutafuta njia sahihi.
Inter Milan:
Baada ya kushuka dimbani
mara 22, ina pointi 29 ikiwa katika nafasi ya 10. Hii ni baada ya kushinda
mechi saba, sare nane na kupoteza saba.
Kwa upande wa takwimu za
mabao, washambuliaji wake wamefunga mabao 33 wakati kinara wa Serie A, Juventus
ana 47.
Angalia, mabao ya kufunga
ni hayo 33, lakini utaona kuwa ina safu nyanya ya ulinzi baada ya kuruhusu
kufungwa mara 29, ikiwa ni tofauti ya mabao manne tu.
AC Milan:
Iko katika nafasi ya 11,
katika mechi zake tano zilizopita imeshinda moja, sare moja na kupoteza tatu.
Rekodi inaonyesha katika mechi 22 ilizocheza imeshinda saba, sare nane na
kupoteza saba.
Wakati safu ya ushambuliaji
ya AS Roma iliyo katika nafasi ya pili ikiwa imefunga mabao 36, AC Milan
imejikongoja na kufikisha 32, lakini ushindi ndiyo tatizo kwao.
Kwa upande wa mabao ya
kufunga, AC Milan nao wametikisa nyavu mara 32 na kufungwa 29, ikiwa na tofauti
ya mabao manne tu.
Kwa mwendo wa timu zote
mbili, kamwe hauwezi kuzipigia hesabu ya kushinda mechi 10 kati ya 16
zilizobakiza.
Hata kama watashinda nusu
ya mechi hizo, mfano washinde nane, watakusanya pointi 24, ambazo ukijumlisha
na walizonazo sasa watakuwa na pointi 53 ambazo sasa Juventus tayari
wamefikisha.
Kwa mwendo wa Juventus,
kama itashinda mechi tano tu, itakuwa na uhakika wa asilimia mia, haiwezi
kufikiwa na timu yoyote.
Swali la kujiuliza giza
lililotamba jijini Milan chanzo chake ni nini? Maana lilikuwa linajulikana kama
jiji la soka!
Sasa limebaki kuwa jiji la
wanamitindo na mambo si mazuri kwa timu zake za soka zenye majina makubwa zilivyokuwa
zinafanya hapo awali na sasa ni aibu tu. Soka limeikimbia Milan.









0 COMMENTS:
Post a Comment