Na Saleh Ally
LIGI Kuu England imebakiza
mechi 13 kwa kila timu itakuwa imefikia tamati huku Chelsea na Manchester City
zikifukuzana kuwania taji la England.
Ukiwauliza mashabiki wengi
katika mitaa mbalimbali ya majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na
mikoa mingine watakuambia timu ambayo inaonekana kuyumba zaidi ni Manchester
United.
Mvuto umepotea na
inaonekana kutokuwa na lile soka la kukata na shoka. Lakini wengi hawaoni Man
United inavyokwenda mwendo wa kimyakimya lakini ni wa kasi kubwa.
Man United bado wanaonekana
ni hatari, hilo linathibitishwa na takwimu na si suala la hadithi au kuamini tu
wamekwisha.
Hadi sasa wako katika
nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 47, tofauti ya pointi tano tu na
wapinzani wao Man City wenye pointi 52.
Kuna uwezekano mkubwa wa
Man United ikawashangaza wengi kwa kumaliza ligi hata ikiwa katika nafasi ya
pili. Kweli, hakuna ubishi ina upinzani mkubwa sana kutoka kwa Southampton
yenye pointi 46 katika nafasi ya nne na Arsenal iliyo na alama 45 nafasi ya
sita.
Kuanzia nafasi ya tatu hadi
ya tano, mmoja akiteleza kidogo, mwingine anakwea. Lakini bado Man United ina
nafasi ya kwenda nafasi ya pili hasa kama Man City itapoteza mechi moja na kutoka
sare moja huku Man United ikishinda zote mbili.
Mwenendo wa Man United
katika mechi tano zilizopita unaonyesha kuwa wa juu zaidi kuliko hata wa Man
City, labda kama baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Stoke City itakuwa
imeamka.
Katika mechi tano zilizopita,
Man City imeshinda moja, sare tatu na kupoteza moja. Wakati Man United
imeshinda tatu, sare moja na kupoteza moja.
Iwapo Man United itaweza
kushikilia rekodi zake na kuendelea kufanya vizuri, itakuwa mtihani kwa Man
City na kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza nafasi hiyo ya pili kwa Mashetani hao
wekundu wanaokwenda mwendo wa kimyakimya lakini wanasonga tu.
Kwa mwendo huo, utagundua
kishabiki, Man United imekwama na haifanyi vizuri. Ila imepoteza yale yaliyozoeleka
lakini bado haijaingia kwenye kundi la Liverpool na bado zikiwa zimebaki mechi
13, iko juu ya Arsenal ambayo bado inaonekana haifanyi vibaya sana.
Mazoea ya nafasi ndiyo
tatizo hapa. Kwamba Arsenal kushika nafasi ya nne au tatu ndiyo kawaida, wakati
United inajulikana kwa ubingwa na nafasi ya pili.
Ugumu zaidi kwa Man United
ni zile mechi 13 zilizobaki, watalazimika kuzicheza kama karata kwa umakini
mkubwa kwa kuwa wana mechi 6 tu nyumba na 7 zilizobaki ni ugenini.
Kwa msimu huu, ushindi
mkubwa kwa Man United ni bao 4-0 dhidi ya QPR na kipigo kikubwa ni bao 5-3
dhidi ya Leicester. Lakini baada ya hapo inaonekana ni bora kwa kuwa imeweza
kucheza mechi nane kabla ya kupoteza, pia imefanikiwa kushinda mara sita
mfululizo.
Hii inaonyesha rekodi zake
bado ziko juu kitakwimu, hivyo Man United bado ni timu isiyotabirika na inaweza
kufanya lolote katika wakati ambao haukutarajiwa.
Iwapo Man United itacheza
vema karata zake 13 zilizobaki angalau wakashinda mechi nane, basi wana nafasi
kubwa ya kuwa katika nafasi ya pili au kubaki hiyo ya tatu na kuwapa kazi ngumu
Arsenal, Southampton na Tottenham kugombea nafasi moja iliyobaki kukamilisha
Top 4 kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mechi:
Cheza 25
Bado 13
Zilizobaki:
Nyumbani 6
Ugenini 7
Ngumu:
Nyumbani: Vs Spurs, Man
City, Arsenal
Ugenini: Vs Liverpool,
Chelsea, Everton
MECHI 13 ZILIZOBAKI:
Februari
21
Swansea V Man Utd
Februari
28
Man Utd V Sunderland
Machi
4
Newcastle V Man Utd
Machi 15
Man Utd V Tottenham
Machi 22
Liverpool V Man Utd
Aprili 4
Man Utd V Aston Villa
Aprili 11
Man Utd V Man City
Aprili 18
Chelsea V Man Utd
Aprili 25
Everton V Man Utd
Mei 2
Man Utd V West Brom
Mei 9
Crystal Palace V Man Utd
Mei 16
Man Utd V Arsenal
Mei 24
Hull V Man Utd










0 COMMENTS:
Post a Comment