Mshambuliaji mwenye kasi wa Yanga, Mrisho
Khalfan Ngassa ameibuka shujaa baada ya kuifungia Yanga mabao mawili katika
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Yanga imelipa kisasi kwa kuichapa Mtibwa
Sugar kwa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar. Katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo, Mtibwa iliichapa Yanga
kwa idadi hiyo mjini Morogoro.
Kwa ushindi huo sasa Yanga imekwea kileleni
kwa kuwa na pointi 25 ikiiacha Azam yenye 22, lakini ikiwa na mchezo mmoja
mkononi.
Ngassa ameibuka shujaa katika mechi ya leo
ameingia katika dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Kpah Sherman aliyechemsha leo.
Dakika hiyohiyo aliyoingia, Ngassa alipiga
mpira uliogonga mwamba wa juu.
Dakika mbili baadaye aliandika bao la kwanza
baada ya krosi safi ya chinichini ya Simon Msuva kumfikia Amissi Tambwe, akiwa
langoni, akashindwa kuunganisha. Yeye akaimalizia kazi hiyo.
Kama hiyo haitoshi, dakika ya 62, Ngassa
alifunga bao la pili kwa kumchambua kipa Said Nduda baada ya pasi safi ya
kupenyeza ya Haruna Niyonzima.
Baada ya bao hilo, Yanga walionekana kucheza
vizuri zaidi huku Niyonzima na Coutinho wakionyesha kutawala zaidi katikati na
Msuva na Ngassa wakizidi kuwasumbua mabeki wa Mtibwa kutokana na kasi yao kuwa
kubwa.
Juhudi za beki Salim Mbonde, zilisaidia kwa
kiasi kikubwa Yanga kutoongeza bao jingine.
Mara kadhaa, Mtibwa Sugar walifika langoni
lakini wakashindwa kuzitumia nafasi zake kutokana na papara za washambuliaji
wake akiwemo Ame Ally ‘Zungu’.
0 COMMENTS:
Post a Comment