Kocha wa Simba, Goran Kopunovic, amempa
masharti magumu beki wa timu yake hiyo, Joseph Owino ambaye amerejea uwanjani
hivi karibuni baada ya kukaa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na majeraha
ya nyama paja.
Owino alianza mazoezi mepesi wiki iliyopita na
anatarajiwa kuanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake hivi karibuni, hivyo
akirudi kikosini kutakuwa na vita kubwa ya namba kati yake na mabeki Hassan
Isihaka na Juuko Murshid ambao kwa sasa wapo kwenye kiwango kizuri.
Kopunovic amesema hawezi kumpa nafasi kwa kuwa anahitaji kuangalia kiwango chake na
nidhamu kabla ya kumpa nafasi ya kucheza licha ya kuwa Owino alikuwa nahodha wa
timu hiyo kabla kocha huyo hajatua klabuni hapo.
“Owino ana nafasi ya kucheza japo mabeki wote
wapo katika viwango vizuri, lakini siwezi kusema namhakikishia namba kwa sasa,
lazima aonyeshe kiwango.
“Sipendi kumuona beki ambaye katika kila mchezo
anapewa kadi au kusababisha penalti, kama hatakuwa na tabia hizo basi ana
nafasi kubwa ya kucheza,” alisema Kopunovic.







0 COMMENTS:
Post a Comment