Timu ya Yanga imewakaribisha wapinzani wao BDF
XI ya Botswana, kuja kuangalia mbinu na mazoezi yao yanayoendelea kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar kwa ajili ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa
Jumamosi hii.
BDF inayoshikilia nafasi ya tatu kwenye Ligi
Kuu ya Botswana, inatarajiwa kuwasili nchini ndani ya siku mbili hizi kwa ajili
ya mchezo wao, kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Gaborone, Botswana kati
ya Februari 27, 28 au Machi Mosi, mwaka huu.
Ofisa
Habari wa Yanga, Jerry Muro, amesema kuwa timu hiyo haina hofu kama wapinzani
wao watakuja kuangalia mazoezi yao kwa kuwa wao wanajiamini na wanacheza soka
la kisasa la kutojificha kwa ajili ya kuhofia wapinzani.
“Hatutawazuia wapinzani kama watataka kuja
kuangalia mazoezi ya timu yetu, ni rafiki zetu, ukiachilia mbali kwamba ni
wapinzani wetu, timu nyingine zimekuwa zikikataza wapinzani kuangalia mazoezi
yao lakini sisi hatupo hivyo, tunacheza soka la kisasa na hatuna wasiwasi
katika kuunda mipango yetu katika uwanja wa wazi.
“Kama watahitaji kuja kutuangalia,
tunawakaribisha kwa kweli wawalete mazoezini, lakini tuseme tu kwamba
tunaliamini zaidi benchi letu la ufundi na kikosi kizima na tunaamini
watatuletea ushindi siku hiyo, hivyo mashabiki na wanachama wote wa Yanga
wajitokeze siku ya mchezo huo kwa ajili ya kuiunga mkono timu yao,” alisema
Muro.
Kwa sasa Yanga ipo kambini kwenye Hoteli ya
Tansoma iliyopo katikati ya Jiji la Dar, huku ikiendelea na ratiba yake ya
mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa kwa wiki yote hii.
0 COMMENTS:
Post a Comment