Kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu,
amewasha honi, juzi aliifungia timu yake mabao matatu ‘hat trick’ kwenye Ligi
Kuu Bara na sasa anasema anaisubiri Yanga kwa hamu.
Ajibu alifunga mabao hayo kwenye ushindi mnono
wa 5-0 dhidi ya maafande waliopoteza dira, Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar na kufikisha jumla ya mabao matano ligi kuu.
Nyota huyo aliyepandishwa akitokea Simba B,
ambaye ndiye mchezaji wa kwanza kufunga hat trick msimu huu, ataivaa Yanga kwa
mara ya kwanza wakati watani hao wa jadi watakapokutana Jumapili ijayo.
Ajibu alisema anasahau maajabu aliyoyafanya dhidi ya Prisons, badala yake anakusanya nguvu kwa ajili ya Yanga.
“Nimejisikia ‘fresh’ kufunga na kuisaidia timu
yangu kusogea juu kwenye msimamo wa ligi, maana lengo letu ni kuchukua ubingwa
msimu huu na hilo linawezekana tukishirikiana kwa pamoja kama timu.
“Mechi inayokuja dhidi ya Yanga ni ngumu zaidi
kwa sababu ina presha sana tofauti na nyingine, kwa sasa ninakusanya nguvu kwa
ajili ya kukutana na Yanga kwa mara ya kwanza kama kocha atanipa nafasi siku
hiyo, maana sijawahi kucheza mechi ya watani,” alieleza Ajibu.
Simba ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi
ikiwa na pointi 23, wakati watani wao Yanga, wanaongoza wakiwa na 31. Katika
mchezo wa kwanza baina ya timu hizo msimu huu, zilitoka suluhu.
0 COMMENTS:
Post a Comment