Baada ya juzi Jumamosi Simba kulala na furaha kutokana na kuipa
kichapo cha mabao 5-0 timu ya Prisons ya Mbeya, jana haikutaka kulaza damu,
badala yake ikasafiri kuelekea Zanzibar kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya
mchezo wao dhidi ya Yanga.
Simba inatarajia kuwavaa mahasimu wao hao wakubwa katika Ligi Kuu
Bara Jumapili ijayo, Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Imekuwa ni kawaida kwa timu hiyo kwenda kuweka kambi visiwani
Zanzibar kila inapokuwa na michezo migumu ya ligi mbele yake, hasa dhidi ya
Yanga. Taarifa zinasema timu hiyo itarejea Jumamosi, tayari kwa mchezo huo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema timu hiyo imeondoka jana majira ya saa sita mchana lakini yeye na Kocha Mkuu, Mserbia, Goran Kopunovic wanatarajia kuondoka leo kujiunga na timu hiyo kutokana na sababu mbalimbali.
“Timu inaondoka leo (jana) na itarejea Jumamosi ila bado hatujajua
kuhusu mechi za kirafiki, lakini kuhusu mimi na kocha Kopunovic, tutaondoka
kesho (leo) kwa kuwa kule mazoezi rasmi yataanza kesho hiyohiyo, ilibidi
tuondoke wote kwa pamoja kesho (leo) lakini ikaangaliwa na uzito wa mechi
yenyewe, tukaona bora timu iwahi kwanza,” alisema Matola.
Katika mchezo wa awali wa ligi, timu hizo zilitoka suluhu lakini
baadaye Simba ilishinda 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe 2.
0 COMMENTS:
Post a Comment