Saleh Ally
JANUARI 2015, uongozi wa Klabu ya Los Angeles Galaxy ya
Marekani ulitangaza kuingia mkataba wa awali wa miezi 18 na kiungo nyota wa
England, Steven George Gerrard.
Usishangae, Gerrard ni nyota wa England kwa maana ya mmoja wa
wachezaji walio na mafanikio makubwa, nadra kufikiwa na wachezaji wengi sana.
Gerrard ni nyota duniani kote, mafanikio yake ni makubwa sana
ukiachana na bahati mbaya yake moja ambayo anaondoka nayo Liverpool mwishoni
mwa msimu huu akiwa hajafanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England.
Mara tatu ameiongoza Liverpool, ameshika nafasi ya pili Ligi
Kuu England 2002, 2009 na 2014. Lakini makombe mengine, yeye kinara.
Amebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja, Kombe la Uefa, mara
moja pia. Uefa Super Cup mara mbili.
Gerard amechukua mara mbili Kombe la FA, Kombe la Ligi, mara
tatu. Hata Ngao ya Jamii nayo kachukua mara moja.
Mechi 497 za ligi akiwa na Liverpool amefunga mabao 117,
hakuna ubishi atafikisha mechi 500 za ligi kabla ya kuondoka. Tayari hivi sasa
katika michuano yote, ameichezea Liver mechi 702 na kufunga mabao 183. Unaweza
kusema amecheza mechi akiwa katika kiwango bora kwa kuwa anaujua mpira,
anajituma, ni mtu anayetaka kushinda.
Katika timu yake ya taifa, amecheza mechi 43 za kirafiki na
kufunga mabao matano, akacheza 50 kuisaidia England kufuzu Kombe la Dunia na
Kombe la Ulaya na kupachika mabao 12.
Katika michuano mikubwa yaani Kombe la Dunia na Kombe la
Ulaya ameichezea England mechi 21 na kufunga mabao manne. Akiwa na timu yake ya
taifa, jumla amecheza mechi 114 na kufunga mara 21.
Gerrard ni mmoja wa wachezaji watakaobaki katika kumbukumbu
za mashabiki wa Liverpool kwa miaka mingine 100.
Nahodha atakayezungumzwa kwa miaka mingine 100, lakini kiungo
mwenye uwezo mkubwa zaidi na gumzo ambaye hatasahaulika hata baada ya miaka 100
ijayo, lakini sasa muda umefika. Wakati ni ukuta.
Mtangazaji mmoja aliwahi kusema ukichagua manahodha wengine
10 ili kuunda kikosi kimoja. Basi Gerrard ataendelea kuwa nahodha wao tena.
Gerrard ana uwezo wa kupiga pasi na mashuti miguu yote, yaani
kulia na kushoto. Amefunga mabao bora zaidi ya 50.
Ana uwezo mkubwa wa kukaba, uwezo mkubwa wa kuchezesha timu
na kubadili mchezo. Ana jicho la kugundua nini sahihi au kipi si sahihi katika
wakati fulani. Lakini leo anaondoka Liverpool.
Anaondoka akiwa amekichezea kikosi cha England kwa miaka 17
mfululizo, alianza kupata namba mwaka 1998, akajihakikishia kikosi cha kwanza
mwaka 2000 na akauchota unahodha akiwa kinda kabisa mwaka 2003. Lakini sasa
anaondoka!
Kwa nini anaondoka kwenda LA Galaxy wakati uwezo na mafanikio
yake yapo kiwango cha juu sana? Jibu ni umri.
Gerrard aliyezaliwa Mei 30, 1980 sasa ana miaka 34. Akiwa
anaichezea Liverpool, utakubaliana nami kuwa uwezo wake uko wazi, bado ni
msaada hata kama anatumika kama kiungo wa chini.
Miaka 34 bado anakaba kwa juhudi, anatoa pasi ndefu kuliko
kiungo mwingine yeyote England. Anafunga mabao na ana uwezo wa kumdhibiti
karibu kila mchezaji bila ya kujali ana umri mdogo au mkubwa. Lakini ameshindwa
kupambana na umri.
Gerrard kaushindwa umri, maana akili yake inataka, mwili
unashindwa kufanya. Pamoja na mafanikio na uwezo wake, ameushindwa umri. Umri
ndiyo umekuwa kiboko yake kama ambavyo umekuwa kiboko ya wengine wengi. Umri
bana, eeh!









0 COMMENTS:
Post a Comment