March 2, 2015


Na Saleh Ally
Nimeandika makala kupitia Kolam ya Metodo nikielezea kuhusiana na kutokuwa na utulivu wa kutosha ndani ya klabu ya Simba.


Makala yangu ilikuwa wazi, najua itakuwa imewagusa wengi na huenda wako ambao hawatafiurahia.

Ndani ya siku moja, nimeamua kuandika makala kwa ajili ya kuweka msisitizo kuhusiana na suala hilo, kwamba Simba wanapaswa kufanya mambo mawili.

Moja ni kukaa na kuzungumza na kupata mwafaka kuhusiana na kile kinachoendelea ambacho ni kutoelewana kati yao, hawana haja ya kuficha.

Kama wakiona imeshindikana, basi wana kila sababu ya kuwekana hadharani, mkorofi, au kama kweli kuna wanamtuhumu na ushahidi wanao, basi wamchukulie hatua.

Katika mkutano wa wanachama uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, asilimia kubwa ya viti vilikuwa wazi.

Viti vilikuwa wazi kwa kuwa idadi ya wanachama iliyojitokeza haikutosheleza. Jiulize kwa nini wanachama hawakuweza kutimia wakati walijua kuna mkutano wa wanachama?

Wanachama hupenda kujitokeza katika mikutano ili kutoa waliyonayo moyoni. Kushindwa kutokea katika mikutano ni dalili mbaya kwa uongozi wa Simba.

Hizo ni dalili kuwa kuna jambo linawakera wanachama wa Simba, wanaumia na huenda ustaarabu wao au hasira zao, ziliwafanya waamue kubaki nyumbani.

Kama wameamua kubaki nyumbani pia ni dalili ya kuchoshwa na mwenendo wa uongozi na huenda siku wakifikia kuzungumza itakuwa mbaya zaidi.

Sasa, lazima uongozi wa Simba ufanye yale mawili wakijua wazi kuwa kilichopo sasa si sahihi kwa kuwa hali halisi inajulikana na uongozi unataka kuficha au unataka kupoza mambo wakati wengi wanajua yalipofikia.

Lengo si kutaka Simba iingie katika migogoro, lakini sahihi ni kuhakikisha inamaliza kila mambo yanayokwenda chinichini halafu si sahihi, yamalizwe.

Simba hawawezi kufanikiwa kama hawaelewani ndani, hauwezi kushinda kama una adui nyumbani kwao.

Adui unayeweza kupambana naye ni yule anayetokea nje. Hivyo nasisitiza, wamalize kama kuna ‘adui’ au wammalize ‘adui’. La sivyo, watashituka mambo yakiwa yameharibika kabisa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic