March 2, 2015



Na Saleh Ally
Wanachama wa Simba wamekutana jana kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam. Lengo lilikuwa ni kujadili mambo mbalimbali ya klabu hiyo.


Katika hali isiyotarajiwa, wanachama hao wamejitokeza kwa idadi ndogo sana, jambo ambalo limeonyesha si dalili nzuri.


Idadi ndogo ya watu, kwangu naichukulia kama kukata tamaa kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, ambao huenda wanaona hawaendani na kiwango walichokitegemea.

Wakati wanachama hao wamejitokeza kwa idadi ya chini, hata mashabiki nao walijitokeza kwa idadi ya chini siku moja kabla, wakati Simba ikiishindilia Prisons kwa mabao 5-0 na kuandika ushindi wake wa kwanza wa kishindo katika Ligi Kuu Bara msimu huu, japokuwa huko mwanzo ilishinda mechi nne.

Tunajua ndani ya Simba kumekuwa kukifukuta. Hata kama mnapinga, lakini inajulikana kuna hali ya mgogoro wa chinichini unaofukuta.

Kumekuwa na hali ya kutoelewana kati ya viongozi na viongozi. Wapo ambao wamekuwa wakituhumiwa kuhujumu timu kwa sababu ya madaraka.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alikuwa kati ya wanaotuhumiwa kuzuiwa kwenda kambini, madai ni mengi ikiwa ni pamoja na suala la kuhujumu timu, tayari Kaburu amelikanusha hilo katika gazeti hili, kwamba si kweli.

Kuna fukuto la mmoja wa viongozi kumsakama Kocha Msaidizi, Selemani Matola, kisa eti alikataa gari lake kukaa mbele katika msafara pia kukataa dawa zake za waganga kupakwa wachezaji.

Matola alitishia hadi kujiuzulu, baadaye suala hilo likazimwa na mwisho wake leo anaendelea kuifundisha Simba. Usisahau, kuna wanachama walijazwa maneno na kumshambulia, lakini hawajui hasa kinachoendelea ndani.


Nani asiyejua kwamba viongozi wa Simba wamewahi kukaa na ‘kumsuta’ kiongozi wa juu, kisa ni kuonyesha kuwa na mwelekeo tofauti na wenzake na walikuwa na ushahidi, akaomba msamaha?

Nani asiyejua kwamba kiongozi fulani wa Simba haelewani na wenzake, kiongozi mwingine pia hapatani na mmoja wao, hivyo kufanya kuwe na hali ya sintofahamu kila wakati.

Angalia hili, wako viongozi wamekuwa wakilalama huku na kule kuhusiana na wenzao. Wapo wenye hoja, wapo wanaopepesa maneno tu lakini ili mradi.

Sasa katika mkutano wa jana, Rais wa Simba, Evans Aveva na Kaburu, waliamua kuwapigia gitaa wanachama wao kwamba hali ni shwari na tulivu. Kwangu naweza kusema si jambo baya kwa kuwa wameamua kufunika kombe, huenda kwa kuwa wana mechi ngumu dhidi ya Yanga inakuja mbele yao.

Hakuna anayeweza kukataa, hata wao Aveva na Kaburu wakati wanazungumza, wanajua kuna matatizo lukuki ikiwemo baadhi ya viongozi kutoelewana na kutuhumiana.

Walipaswa kuwa wakweli, kama wameamua kuficha basi lazima wakubali huu ndiyo wakati mwafaka wa kulimaliza suala hilo la kulumbana au chuki baina yao, la sivyo, itafikia siku wataaibika na mimi nitawakumbuka.

Kaburu kaonyesha hana tatizo na Aveva, pia Aveva hali kadhalika kwa Kaburu. Kitu ambacho nasisitiza, wanachama wameondoka wakiwa wameamini waliyoambiwa na viongozi wao na haitakuwa busara wakisikia tena kimefumuka kitu kama hicho.

Kuzungumza kwa ajili ya kuweka vizuri hali ya hewa, limekuwa ni jambo zuri kwa ngazi ya kiuongozi. Lakini huenda kusema ukweli lingekuwa jambo zuri zaidi ili wanachama wajadili na mwisho kufikia mwafaka wa kurekebisha mambo.

Kama viongozi waliona vizuri kufunika kombe, basi wawe makini, wakae na kukubaliana, kuwa wamalize tofauti zao ili wasirudi tena katika kile kilichosababisha hali ya kutoelewana.

Simba haiwezi kwenda kwa malumbano ya chuki, kila kuonyesha anajua sana, anajulikana sana au ana fedha nyingi. Pia msisitizo wa suala la heshima kwa maana ya huyu ni kiongozi wa ngazi hii na huyu ngazi ile.

Lakini pia kuwe na uwazi wa kukubali kuambiana. Si mtu akikosolewa kwenye kitu au kikaoni, ananuna milele na kujenga uadui.

1 COMMENTS:

  1. Tuandikie agenda za mkutano, nini kimejadiliwa na maamuz ya mwisho ni yepi... Unatuandikia maoni yako si wengine hayatusaidii... Isitoshe unaandika historia badala ya nn kilichozungumzwa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic