April 8, 2015


Na Saleh Ally
KOCHA Mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho, aliwahi kusema soka ni mchezo wenye matokeo ya kikatili sana. Unaweza kulithibitisha hilo kwa kinachoitokea Mtibwa Sugar sasa!


Katika mechi nane za mwanzo za Ligi Kuu Bara haikupoteza hata moja, tena ikamaliza ikiwa kileleni. Lakini sasa bundi kajenga kiota chake ndani ya kikosi hicho, mambo hayaendi tu, why!

Mtibwa Sugar sasa ni timu inayopambana kuokoa uhai wake ili ibaki Ligi Kuu Bara, msimu ujao! Imebakiza mechi sita.


Mtibwa Sugar wana nini hasa? Tatizo lao ni lipi? Katika mahojiano na gazeti hili, Kocha Mkuu, Mecky Maxime ambaye ni mmoja wa makocha wanaofanya vizuri, anasema:

“Ambacho ninaweza kusema ni kuwa timu bado inacheza vizuri na walioiona katika mechi zote wanaweza kusema. Tatizo letu hatupati matokeo, hatujatumia nafasi.

“Mechi dhidi ya Kagera muda wote tumeshambulia, lakini tukapoteza. Mechi dhidi ya Stand sisi tumecheza vizuri zaidi, wao wamepata nafasi mbili, moja wakaitumia. Hivyo huo ndiyo mpira, lakini tunaendelea kupambana. Mimi najua kipindi hiki yatasemwa mengi sana.

“Nimekuwa mchezaji na sasa kocha, nimezoea maneno kama hayo. Ila kawaida naangalia, anayesema ni nani, kweli anaujua mpira? Wewe leo umepiga simu angalau kusikia kutoka kwangu. Wengine wanaandika tu au kutangaza tu, kitu ambacho si sawa.

“Nasisitiza, wachezaji wangu hawana tatizo, hakuna mgomo, mazoezi tunafanya vizuri, stahiki zetu na kila kitu kinakwenda vizuri. Lakini mpira nao una mambo yake. Tutapambana hadi mwisho,” anasema Maxime ambaye alikuwa beki mahiri wa pembeni wa Mtibwa Sugar, Kili Stars na Taifa Stars.


Ukimsoma vizuri Maxime, ndiyo kile alichokuwa akikizungumza Mourinho kwamba mpira una matokeo ya kikatili. Utajiandaa vizuri, utakuwa unajiamini, utacheza vizuri na mwisho utapoteza.

Lakini Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, yeye anajivunia kwamba katika mechi sita zilizobaki, tano zitachezwa kwenye Uwanja wa Manungu mjini Turiani. Ana imani watakaotia mguu pale watakiona.

Lakini mechi hizo sita, nne watacheza na timu za majeshi, kwamba hazitakuwa rahisi. Mara mbili wanakutana na Prisons, Manungu na Sokoine mjini Mbeya. Timu hiyo ya Magereza nayo inapambana kuepuka kuteremka daraja.

Mechi mbili nyingine ni dhidi ya timu nyingine za majeshi; JKT Ruvu na Ruvu Shooting ambazo zinahitaji ushindi pia kuhakikisha zinabaki katika ligi hiyo.

Mechi mbili za timu zisizomilikiwa na majeshi ni dhidi ya Azam FC wanaowania kutetea ubingwa wao au kupata nafasi ya pili, halafu Coastal Union yenye pointi 24, hivyo inahitaji ushindi ili isiteleze na kuteremka wakati inajua watani wao African Sports tayari wametua ligi kuu.

Hii ni sehemu ya kuonyesha ugumu tena usiopimika kwa Mtibwa Sugar kutokana na inavyokwenda. Tangu Januari 25 hadi leo, Mtibwa imeshinda mechi moja tu! Kwa hali ilivyo, ingawa inaonekana kama mzaha, kama Mtibwa itapoteza mechi tatu zijazo, safari ya kuteremka daraja itakuwa imewadia.

Kinachoshangaza zaidi kwa Mtibwa ni kuwa timu ambayo haikupoteza hata mechi moja katika nane za kwanza kabla ya mapumziko marefu hadi kufungwa mara saba katika michezo 12 iliyocheza baada ya hapo.

Hali ilivyo, kama Maxime anakiamini kikosi chake kama alivyozungumza mwenyewe. Basi kuna kila sababu ya kuwekeza nguvu nyingi katika saikolojia.

Huu ndiyo wakati wa kuwaambia wachezaji kwamba kweli wameteleza, lakini sasa ni wakati mwafaka wa kurudi na kuhakikisha angalau wanapata pointi 12 ili kuepuka aibu ya kuteremka daraja.

 MSIMAMO:


                            P         W         D         L           F           A         GD           PTS       

1. Yanga         19         12         4         3         28         11         17         40       

2. Azam         18         10         6         2         25         12         13         36        

3. Simba         21         9         8         4         27         15         12         35       

4. Kagera         21         7         7         7         19         20         -1         28       

5. Ruvu                     21         6         8         7         14         18         -4         26       

6. Coastal         21         5         9         7         14         15         -1         24       

7. Mbeya         20         5         9         6         15         17         -2         24       

8. JKT               21         6         6         9         16         20         -4         24       

9. Stand         20         6         6         8         17         23         -6         24       

10. Mgambo19         7         3         9         13         19         -6         24       

11. Ndanda 21         6         6         9         18         25         -7         24       

12. Mtibwa         20         5         8         7         19         21         -2         23       

13. Polisi         20         4         9         7         13         17         -4         21       

14. Prisons         20         3         9         6         14         20         -6         20       



MECHI ZILIZOBAKI:

Aprili 11, 2015

Mtibwa         v         Azam                           Manungu





Aprili 15, 2015

Mtibwa         v         Prisons                  Jamhuri





Aprili 19, 2015

Prisons         v                  Mtibwa                  Sokoine





Aprili 26, 2015

Mtibwa         v                  JKT                  Manungu


Mei 3, 2015

Mtibwa         v                  Ruvu                           Manungu


Mei 9, 2015

Mtibwa         v                  Coastal                  Manungu


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic