Suala la usajili wa
mshambuliaji wa kimataifa wa Azam, Mrundi, Didier Kavumbagu, imechukua sura
mpya baada ya kutoa kipindi cha muda wa mwezi mmoja ambapo ni sawa na siku 30,
kabla hajajua kama atajiunga na Yanga ama la.
Kavumbagu ambaye amekuwa
lulu katika kikosi cha Azam tangu atue msimu huu klabuni hapo akitokea Yanga,
amekuwa akihusishwa mara kwa mara kurejea Jangwani, huku ikidaiwa kuwa tayari
kuna mazungumzo ya siri kubwa yameanza baina yake na vigogo wa Yanga lakini
yeye akasisitiza kutoa mwezi mmoja kabla ya kutangaza ameamua anakwenda wapi
kwa ajili ya msimu ujao.
Mpaka sasa Kavumbagu
amebakiza takriban miezi miwili ili kumaliza mkataba wake na Azam FC ambayo
ilimsajili na kumpa mkataba wa mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa kanuni za
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji huyo kwa sasa anaruhusiwa
kufanya mazungumzo na timu nyingine yoyote.
Kavumbagu amesema kuwa hilo suala la kutakiwa na Yanga amekuwa
akilisikia lakini kwa sasa hawezi kulitolea sana ufafanuzi kwa kuwa bado
anaendelea kutafakari na kisha baada ya kipindi cha mwezi mmoja kupita, atakuwa
tayari ameshajua muelekeo wake na kila mmoja atafahamu kuwa atakuwa wapi msimu
ujao.
Aidha, Kavumbagu aliyefunga
mabao 10 mpaka sasa kwenye ligi akizidiwa moja na kinara Simon Msuva wa Yanga
mwenye 11, ameongeza kuwa anaamini kipindi cha mwezi mmoja kinamtosha zaidi
kuisaidia Azam katika kuubakiza ubingwa Chamazi kisha baada ya hapo na yeye ndiyo
atageukia upande wa pili na kuangalia zaidi maslahi yake.
“Kwa sasa siwezi kuwa na
jibu la moja kwa moja kuhusiana na Yanga au Azam kwa sababu bado kuna muda
zaidi hapa katikati na baada ya mwezi mmoja nitakuwa tayari nimeshapata jibu
kichwani kama nitabaki Azam au nitakwenda Yanga au sehemu nyingine.
“Kwa sasa nataka kutoa sana
msaada kwa timu yangu ya Azam kuhakikisha tunautetea ubingwa msimu huu na
kipindi cha mwezi mmoja kinatosha kabisa kufanya hivyo.
“Kwa sababu baada ya mwezi
zitakuwa zimebaki kama mechi mbili kumalizika kwa ligi na kama ni nani anatwaa
ubingwa itakuwa tayari imeanza kubainika, kwa hiyo na mimi sasa hapo naweza
kuangalia mambo yangu ya msimu ujao kuona itakuwaje, niamini nachokwambia
kwamba baada ya muda huo kila kitu kitakuwa wazi na hakutakuwa na maswali
mengine tena,” alisema Kavumbagu.
Pamoja na hayo lakini Yanga
inaonekana kuwa na asilimia nyingi zaidi za kumrejesha mchezaji wao huyo
waliyemsajili kwa mara ya kwanza msimu wa 2012/13 akitokea Atletico ya Burundi
baada ya kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, kukiri kuwa ‘target’ zake
katika usajili huu ni kupata straika mwenye vigezo kama alivyonavyo Kavumbagu
kwa ajili ya kukisaidia kikosi chake kwenye mapambano ya msimu ujao.
Hata hivyo, mbali na hayo,
mashabiki wa Yanga pia wameonyesha hali ya kuhitaji huduma ya straika wao huyo
baada ya kumueleza wazi kumtaka arudi nyumbani walipokutana naye jijini Tanga,
Yanga ilipokuwa ikiumana na Mgambo Shooting na Azam ilipokwenda kucheza na
Coastal Union.
Kwa upande mwingine Azam leo
itapata pigo kwa kumkosa mshambuliaji wake huyo katika mchezo wao dhidi ya
Mbeya City utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar kutokana na kuwa na kadi
tatu za njano.
0 COMMENTS:
Post a Comment