April 25, 2015



Na Saleh Ally
UKICHUKUA listi ya wanamichezo 100 wanaolipwa zaidi duniani kwa mwaka, utagundua kweli michezo inalipa.
Rekodi inaonyesha hivi, katika wanamichezo 100 wanaolipwa zaidi duniani, anayecheza kriketi ni mmoja, michezo ya ndani kama riadha ni mmoja, ngumi wanne, gofu watano, tenisi watu sita kama ilivyo kwa madereva wa mashindano ya magari.

Soka la Marekani wapo 15, mpira wa miguu 17, kikapu wachezaji 18 na mpira wa magongo wachezaji 27, hii ni kwa mujibu wa Forbes.
Katika hao 100, wanawake ni watatu tu ambao ni Maria Sharapova akiwa namba 34 (anaingiza dola milioni 24.4), Li Na aliye nafasi ya 41 (dola 23.6m) na Serena Williams katika nafasi ya 55 (dola 22m).

Kinachovutia zaidi katika hilo, pamoja na umaarufu wao na uingizaji wa fedha, lakini kuna pengo kubwa sana namna fedha hizo zinavyoingia.

Mfano mzuri, unaweza ukachukua katika michezo maarufu zaidi duniani bila kujali unazungumzia Afrika, Ulaya, Amerika Kusini au Asia, ambayo ni soka na ngumi.

Mchezo wa ngumi ambao zaidi unatumia mikono, ndiyo una mwanamichezo anayeongoza kwa kuchota fedha nyingi zaidi ambaye ni Floyd Mayweather.
 
RONALDO
Ukienda kwenye listi ya wachezaji watano wanaochota fedha nyingi zaidi kwa mwaka, ngumi ina mmoja, soka wawili na kikapu wawili. Kama ni aina ya michezo, basi miguu ni watu wawili ambao ni Cristiano Ronaldo na Lionel Messi na mikono ni watatu ambao ni Mayweather, Lebron James na Kobe Bryant.

Utamu unakuja katika namna ya uingizaji fedha hizo, twende sasa katika ngumi na soka halafu uone. Mayweather na Ronaldo au Messi, kuna utamu wake.

Mwaka jana, Mayweather alicheza mapambano mawili, akafanikiwa kuingiza dola milioni 105. Wakati Ronaldo akiwa amecheza zaidi ya mechi 50 na akafanikiwa kuingiza dola milioni 80 (Sh bilioni 155)!

Katika pambano moja, Mayweather alicheza raundi 12. Kila raundi ni dakika tatu, maana yake pambano moja alitumia dakika 36.
MESSI
Katika mapambano yake mawili, alitumia dakika 72 tu kuingiza dola milioni 105 (Sh bilioni 203). Maana yake kama Ronaldo alicheza mechi zaidi ya 50 kuingiza dola milioni 80, Mayweather kama ingekuwa soka, maana yake hakumaliza hata mechi moja!

Utamu zaidi uko hapa. Pambano la ngumi linakuja, huenda litakuwa maarufu kuliko yote duniani na linawakutanisha Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao na litapigwa Mei 3.

Malipo yake yapo juu zaidi na katika fedha dola milioni 300, Mayweather atachukua 60% ambazo ni dola milioni 180 (Sh bilioni 348) na Pacquiao atabeba 40% ambazo ni dola milioni 120 (Sh bilioni 232).

Fedha anazolipwa Mayweather katika pambano hilo inabaki kidogo tu ifikie fedha anazolipwa Messi kwa miaka mitatu ambapo anatarajia kuingiza dola milioni 195 ambazo pia zinaweza kushuka au kupanda kulingana na anacheza vipi kwa michezo ijayo.

Tena Mayweather anaweza kuingiza fedha hizo katika dakika 36 ambazo hazifikii hata kipindi kimoja cha mechi moja ya soka.

Kweli michezo ya miguu kama soka inapendwa zaidi, lakini michezo ambayo mikono ndiyo ‘kitumio’ namba moja ndiyo inalipa zaidi, mfano mzuri ni huo mlinganisho wa Mayweather dhidi ya Ronaldo na Messi ambao ndiyo wanasoka wanaochota fedha rundo kuliko wengine wote.
Kwa hapa nyumbani mambo bado yanaonekana si mazuri sana kwa mabondia kwa kuwa wengi wanalipwa kidogo na mchezo umekuwa hauna watu wengi wa kweli wanaoweza kuufanya ukue na kufika mbali zaidi.
Angalau soka, kuna wachezaji wanaolipwa hadi dola 4,000 (Sh milioni 7.7) kwa mwezi. Hata huko kuna matatizo kibao kwa kuwa wajanja wanaoshibisha matumbo yao, wapo rundo.

TANO BORA YA WANAMICHEZO WANAOLIPWA ZAIDI:
1. Floyd Mayweather        dola milioni 105
2. Cristiano Ronaldo          dola milioni    80
3. LeBron James                 dola milioni    72
4. Lionel Messi                     dola milioni   65

5. Kobe Bryant                    dola milioni    62

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic