April 25, 2015

MADRID

Na Saleh Ally
HISPANIA wanaendelea kutawala katika michuano mikubwa barani Ulaya kwa upande wa klabu kwa kuwa safari hii katika hatua ya nusu fainali yenye timu nne, wao wameingiza mbili kama kawaida yao.


Real Madrid ambao ni mabingwa watetezi na Barcelona wenye uchu wa juu kulitwaa kombe hilo. Sasa ni vita dhidi ya timu mbili, Bayern Munich kutoka Ujerumani na Juventus ya Italia.

Raha zaidi, hata Bayern nayo inafundishwa na kocha wa zamani wa Barcelona pia ni raia wa Hispania, huyu ni Pep Guardiola. Hii inaonyesha Hispania ina nafasi ya kusherekea kombe hilo kwa namna yoyote.
 
BAYERN
Kama timu zake mbili zitaingia fainali, basi limebaki Hispania. Kama itaingia moja dhidi ya Bayern, bado wana nafasi ya kuendelea kusherekea hata kama litaenda Ujerumani. Watalikosa iwapo litachukuliwa na Juventus.

Katika droo ya jana, mabingwa watetezi Real Madrid walipangwa kucheza na Juventus, Barcelona walipangwa kukutana Bayern Munich. 
 
BARCELONAKwa maana ya ubora inaonekana ni kazi kubwa Juventus kuzipiku timu hizo tatu za Bayern, Barcelona na mabingwa watetezi Real Madrid, lakini soka nalo “hupanga” yake, hivyo usishangae kwa lolote.

Tayari imeshajulikana nani atacheza na nani katika nusu fainali hizo mbili. Mechi za kwanza zitachezwa Mei 5 na 6 na zitarudiana Mei 12 na 13.
 
JUVENTUS
Kwa kuwa ni timu nne bora za Ulaya, uhakika yoyote inaweza kukutana na nyingine. Maana yake hakuna atakayekuwa na hofu ingawa taarifa zinaeleza kila mmoja kati ya timu hizo tatu, alikuwa akitamani kukutana na Juventus anayeonekana mnyonge kitakwimu.

Takwimu zinaibeba Barcelona kama timu bora zaidi katika hizo nne zinazokutana kama utaangalia mechi zote kuanzia hatua ya makundi hadi robo fainali.

Kila timu imecheza mechi 10 na Barcelona inaonekana kufanya vizuri zaidi katika nyanja mbili tatu. Madrid na Bayern nazo zina sehemu zake zimeonyesha ubora wake.

Katika mechi hizo 10, Barcelona imeshinda tisa, imepoteza moja na kama utatengeneza msimamo inakuwa juu zaidi ya nyingine kwa kuwa na pointi 27 sababu haina sare hata moja.

Real Madrid inashika nafasi ya pili ikiwa imeshinda nane, sare moja na kupoteza moja na ina pointi 25 lakini inaonekana kuwa na safu ngumu zaidi ya ulinzi kwa kuwa imefungwa mabao sita tu huku Barcelona ikiwa imeruhusu mabao saba na Bayern mabao manane.

Bayern inashika nafasi ya tatu kwa ubora ikiwa imeshinda mechi saba, sare moja na imepoteza moja. Imekusanya pointi 22 lakini ndiyo timu yenye safu kali zaidi ya ushambuliaji baada ya kufunga mabao 30, ikifuatiwa na FC Porto yenye 25, Barcelona yenye 23 na Madrid iliyofunga 22.

Juventus inashika nafasi ya tano kwa ubora nyuma ya Porto iliyo nafasi ya nne. Timu hiyo ya Italia imeshinda mechi sita, sare mbili na imepoteza mbili na kukusanya pointi 20.

Ukiuangalia msimamo wa ubora unatoa majibu mengi magumu kulingana na hali jinsi ilivyo na inakuwa vigumu sana kuamua nani anaweza kumshinda nani atakapokutana naye katika hatua ya nusu fainali.

Pamoja na ubora wa rekodi hizo kwenye msimamo, bado inaonekana kila timu ina sehemu bora zaidi ya nyingine na kama itarejirekebisha kutokana na makosa ya mechi mbili za robo fainali, basi inaweza kuwa na ubora zaidi.

Bado ni vigumu sana kusema timu gani itaingia fainali kutokana na hali halisi kwa kuwa hakuna inayoonyesha kuwa na ubora wa asilimia 60 kuzidi nyingine.

Ubora ni wa kugawana, hivyo hata Juventus yenye ubora nafasi ya tano imeingia katika nafasi ya nne. Hii inaonyesha bado Juventus inaweza kuendelea kushangaza na kuwaacha nyuma wanaoidharau kwamba haifai au ni dhaifu kuliko timu nyingine tatu zilizofuzu.

Mfano katika ubora wa mabao, timu inaweza kufunga wakati gani, kipindi cha kwanza chenye dakika kuanzia 1-45 au cha pili kinachoanzia 46-90, inaonekana kila moja ina ubora wake pia.

Bayern wanaendelea kuwa juu kwenye ubora wa ufungaji pia ni wabaya zaidi kipindi cha kwanza ambacho wamefunga asilimia 60 ya mabao yao na kipindi cha pili wakafunga kwa asilimia 40.

Barcelona nao wanaonekana ni wabaya pia katika kipindi hicho cha kwanza kwa kuwa 65.2% ya mabao yao yamefungwa kipindi cha kwanza pia na cha pili wamefunga kwa 34.8%.

Real Madrid hawako mbali, hawatofautiani na wenzao kwa kuwa nao wakali katika kipindi cha kwanza kwani wamefunga mabao yao kwa 68.2% na kipindi cha pili kwa 31.8%

Juventus wako mbali sana, ingawa ndiyo timu tofauti katika hizi nne zilizoingia nusu fainali kwani wakali zaidi katika kipindi cha pili kwa kuwa wamefunga mabao yao kwa 69.2% wakati kipindi cha kwanza ndiyo wamefunga kwa 30.8%.

Unaweza ukabashiri kwa urahisi sana kutokana na timu unavyozijua lakini hadi sasa kombe hilo halina mwenyewe kwa kuwa kweli timu hizo nne ni ‘cream’ ya Ulaya na zina wachezaji wa kila aina wanaoweza kubadilisha matokeo si kwa mfumo, badala yake ni uwezo wao binafsi walionao.

MSIMAMO WA UBORA:
                                 P         W            D         L         GF         GA         Pts       
1. Barcelona          10           9            0          1         23         7         27       
2. Real Madrid      10            8            1         1         22         6         25       
3. Bayern              10             7            1         2         30         8         22       
4. FC Porto           10            6             3         1         25         12         21       
5. Juventus           10             6             2         2         13         5         20       
6.  A. Madrid        10            5             2         3         15         5         17       
7. Chelsea              8             4             4         0         20         6         16       
8.  Arsenal             8             5              1         2         18        11       16       
9. Monaco            10            4               3         3         7         5          15       
10. Paris SG         10            4              3          3         14      15         15       


MSIMAMO WA MABAO:
                             MABAO    DK 1-45          DK 46-90
Bayern Munich         30         60.0%                  40.0%       
FC Porto                    25         28.0%                  72.0%       
FC Barcelona           23         65.2%                    34.8%       
Real Madrid             22         68.2%                     31.8%       
Chelsea                     20         55.0%                     45.0%       
Arsenal                     18         55.6%                    44.4%       
Shakhtar                   15         46.7%                    53.3%       
Atletico Madrid        15         33.3%                    66.7%       
Dortmund                 15         46.7%                    53.3%        
Paris SG                   14         42.9%                    57.1%       
Juventus                   13         30.8%                    69.2%  



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic