OKWI WAKATI AKIICHEZEA ETOILE DU SAHEL |
Na Saleh Ally
INAWEZEKANA wengi wamekuwa wakijaribu kupotosha hoja ya
msingi ya kile ambacho nimekuwa nikikizungumzia kuhusiana na biashara ya mchezaji
Emmanuel Okwi iliyofanyika kati ya Simba na Etoile du Sahel.
Huenda kuna kila sababu ya kushikilia na kusisitiza kile
ambacho nimekuwa nikikielezea kwamba Okwi aliuzwa ‘bure’ na Simba ilifanya
biashara ‘kichaa’. Ilimuuza kwa dola 300,000 (Sh milioni 480), hadi sasa
haijawahi kulipwa hata senti!
Wiki iliyopita nilionyeshwa mwandishi mmoja alizungumza
na Rais wa Etoile du Sahel, Charefeddine Ridha na swali lake la msingi lilikuwa
ni kumuuliza kama kweli walifanya dili yeye na Mwenyekiti wa Simba wakati huo,
Ismail Aden Rage, yaani huenda alipewa chochote.
Jibu la rais huyo wa Etoile lilikuwa “hapana”, huku
akisisitiza wao hufanya mambo yao kwa unyoofu. Nikashangazwa na “akili” ya
mwandishi, kweli alitegemea jibu la “kweli tulimlipa fulani dili”. Ingekuwa
kichekesho!
Tena mbaya zaidi, eti rais huyo akasema Rage
anachafuliwa tu! Utajiuliza anajua nini kuhusiana na hilo, eti anachafuliwa!
Kweli watu wenye akili zao timamu wanaweza kusifia katika hilo!
Nikaachana na hilo, sikutaka kuwa kwenye kundi la kuwaridhisha
watu kwa kuwa najua gazeti ninalolitumikia ni gazeti la wasomaji, si kwa ajili
ya kuridhisha watu hata kama wamefanya madudu. Pia naepuka kuwa kwenye kundi la
wanaoandika kwa mtindo wa “gari la mkaa”. Leo shamba, kesho gereji.
Msisitizo unabaki palepale, mambo ya kuchafuliwa yawekwe
kando na anayepinga kwamba Simba hawakufanya biashara ya kichaa anyooshe mkono,
atoe hoja za msingi. Hakuna ubishi Rage alifanya makosa.
Alifanya biashara mali kauli, akakubali kutoa uhamisho
wa Okwi, Simba ikiwa haijalipwa hata senti. Hili ndiyo nimekuwa nikisisitiza,
suala la alipewa au hakupewa cha pembeni mimi silijui, linabaki kuwa siri yake.
Ila maswali yanaongezeka kutokana na alivyoshiriki katika suala hilo na
lilivyokwenda, majibu anayo mwenyewe.
Ndiyo maana suala hili naliona kama vile ni Simba na
Etoile wanacheza disco. Dj anapiga muziki uleule, lakini anatudanganya kwa
kutubadilishia rangi ya CD tu! Wenyewe tuko ‘busy’ tunashindana kucheza.
Fedha wanazotakiwa kulipwa Simba ziko wapi hadi sasa?
Hata kama Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limesema baada ya kesi hiyo ya
Simba, vipi hadi leo hawajalipwa.
Nataka nikukumbushe msomaji, hata Simba wakilipwa mwezi
ujao, hawatakwepa kauli ya kuwa walifanya biashara kichaa ambayo si mkopo
lakini unakabidhi unachokiuza halafu unakuja kulipwa baada ya miaka mitatu
baadaye.
Watu makini hawawezi kufanya biashara ya “kupapasa” kama
hiyo. Kila kitu kina misingi yake na Simba isingesumbuka leo kwenda Fifa au
kwingineko na badala yake kama kuna tatizo kati ya Okwi dhidi ya Etoile
wangelimaliza wenyewe na si Simba kujumlishwa.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF),
Krifa Jalel aliniambia kwanza alitaka kumuona Okwi ili amhoji kwa nini
aliondoka Tunisia baada ya miezi mitano na ushee.
Akasisitiza, Simba vipi wanataka kulipwa wakati Okwi
yuko Dar es Salaam na anaichezea Simba tena wanajua ameondoka Tunisia bila ya
kufuata utaratibu?
Hili lilinipa picha huenda Simba watalipwa miaka kumi
ijayo, ikiwezekana wameishapita zaidi ya marais wawili madarakani baada ya
Evans Aveva.
Tathmini ya hili linaonekana kuingiliwa na siasa, lakini
ukweli unaonyesha hivi, Simba ya Rage ilichemka katika hili, awe alikuwa akijua
au la.
Mbaya zaidi, alikuwa mkali kila linapozungumziwa suala
hili kwa kisingizio kuwa anasakamwa. Sasa hadi leo wamelipwa? Jibu unalo.
Sasa kutumwa au kusakamwa kunaingia vipi? Jiulize tena,
Etoile walikuwa hapa jijini hakuna kiongozi wa Simba aliyewafuata hata
kuwauliza.
Kweli suala liko Fifa, lakini bado kukutana na viongozi
hao tena rais wa klabu, ingekuwa nafasi nzuri ya kukaa na kuzungumza nao kujua
ukweli angalau kuwashawishi kiungwana na ikiwezekana kujenga urafiki wa mambo
mengine.
Nakumbuka Simba walifunga safari hadi Tunisia kwenda
kuzungumza nao. Wakiwa hapa, hakuna aliyewaona kusisitizia hilo. Sijui,
tusubiri, lakini msisitizo wangu kwa mara nyingine ni huu. “Simba wamefanya
biashara kichaa kwa kumuuza Okwi bure.”
Katika maelezo, hakuna mahari popote ambapo Rage alitia sign au kushiriki katika biashara a Okwi, walioshiriki wanajulikana lakini mbona hawatajwi!! Pili simba walikosea kumsajili Okwi, Etoile wakiwa bado wana kesi ya fifa ya Okwi kutoroka, tayari Okwi ameshazunguka na kurudi Simba!! Etoile wanaona hizo ni njama na kwa vyovyote hata ningekuwa mimi ningejua Simba wameshiriki kumtorosha. Haiwezekani mmeuza mchezaji na kabla hamjalipwa mchezaji ametoroka, hakafu kesho namkuta anacheza kwako bado unasema unanidai!! Itakuwa utaperi basi
ReplyDelete