El Merreikh ya Sudan na Gor Mahia ya
Kenya ni kati ya timu zinazoelekeza nguvu ikiwezekana zimnase beki wa wa Yanga, Mbuyu Twite raia wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo.
Twite, amebakiza si zaidi ya miezi miwili
kabla ya kumaliza mkataba wake Yanga na kwa sheria za Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa), anaruhusiwa kuanza mazungumzo na timu nyingine yoyote kwa
sasa.
Twite amesema kila kitu kuhusiana na matarajio
yake baada ya kumalizika kwa ligi ikiwemo kufafanua kuhusiana na ishu ya
usajili na jinsi mambo yote na mazungumzo yanavyoendelea kwa sasa kwa timu hizo
zinazomuwania.
“Ni kweli kuna timu zimekuja kuzungumza na
mimi, lakini ya kwanza kabisa ilikuwa ni El Merreikh, maofisa wao walinitafuta
walipokuja kucheza na Azam, wakaniambia lengo lao la kunitaka ni kwa ajili ya
kwenda kuziba pengo la beki wao anayetaka kuihama timu hiyo.
“Lakini wa pili walikuwa ni Gor Mahia, wao
walikuja wakasema wananihitaji kwa ajili ya msimu ujao, nikaongezee nguvu
kikosi chao, hakuna timu niliyomalizana nayo kati ya hizo japokuwa tumezungumza
kila kitu, nimewapa ahadi kuwa ligi ikiisha tu wanitafute ndiyo tutajua cha
kufanya na wakakubali.
“Hapa Tanzania zipo pia timu zilizonifuata,
Simba wao walikuja, tulizungumza kidogo lakini lengo lao kubwa lilikuwa ni
Kabange (Twite), nikawarahisishia mawasiliano, waliwasiliana naye na sijajua
sasa hivi wameishia wapi.
“Kiukweli kabisa bado sijafanya maamuzi, kwa
sababu nimeipa kwanza nafasi timu yangu ya Yanga, nawasikiliza wao wanasemaje
kuhusu msimu ujao, kama watanihitaji, tutazungumza kuona kama tutafikia muafaka
lakini ikiwa tofauti basi nitaangalia sehemu nyingine,” alisema Twite.
Pamoja na yote hayo lakini inaonekana kuwa El
Merreikh wapo ‘serious’ katika mpango wao huo kwani siku za nyuma Championi
liliwahi kuzungumza na Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha ambaye alisema kuwa
moja ya barua walizopokea kwa ajili ya kuhitajika kwa wachezaji wao ni kutoka kwa
El Merreikh ingawa hakuwa tayari kufafanua zaidi na kumtaja mchezaji husika
aliyeletewa maombi hayo.
0 COMMENTS:
Post a Comment