Straika wa Yanga, raia wa Burundi, Amissi
Tambwe, ameweka bonge la rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kupiga hat-trick
(mabao matatu mechi moja) tatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mrundi huyo, ni mchezaji pekee aliyeweka
rekodi hiyo ambayo haijawahi kuwekwa na mchezaji yeyote tangu uwanja huo
ulipoanza kutumika.
Tambwe, mechi yake ya kwanza kufunga hat trick
kwenye uwanja huo ilikuwa ni Februari Mosi, 2014 dhidi ya JKT Oljoro akiwa na
Simba ambayo ilishinda 4-0.
Mechi nyingine ambayo Mrundi huyo alifunga hat
trick ilikuwa ni Septemba 19, 2014 dhidi ya Mgambo JKT ambayo timu yake ya
Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0.
Mshambuliaji huyo alikamilisha rekodi yake ya
kupiga hat-trick ya tatu wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa kwa kufunga
mabao manne katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union iliyocheza na
Yanga.
Tambwe aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita
wa ligi kuu akifunga mabao 19, alitua kuichezea Yanga kwenye usajili wa dirisha
dogo msimu huu akitokea Simba baada ya kumsitishia mkataba wake kabla ya kutua
Jangwani.
Upo uwezekano mkubwa wa mshambuliaji huyo
kukitetea kiatu chake cha dhahabu kutokana na kasi yake kubwa aliyonayo hivi
sasa ya kufunga mabao.
Mrundi huyo, hadi hivi sasa amefanikiwa
kufunga mabao 9, akiongozwa na Simon Msuva mwenye 13 akifuatiwa na mshambuliaji
wa Azam FC, Didier Kavumbagu aliyepachika 10 na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar
ambaye naye ana mabao 10.
Kati ya hat-trick hizo alizozipiga, idadi
kubwa ya mabao amefunga kwa kichwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga
aina hiyo ya mabao huku mengine kwa kumchambua kipa.
0 COMMENTS:
Post a Comment