Na Saleh Ally
YANGA sasa inaweza kuwa
mfano ikiwezekana kwa kila klabu kutokana na mwenendo wao mzuri katika kila
eneo.
Hata kama si kwa asilimia
mia, lakini asilimia nyingi zaidi inaonyesha kuna utulivu, ushirikiano na
umoja.
Kwa upande wa timu, Yanga
ndiyo wana kikosi imara zaidi ambacho kina kila dalili ya kuwa bingwa wa
Tanzania Bara na kuipokonya taji Azam FC kama si maajabu ya mpira. Kufikia
hivyo, haiwezi kuwa kazi rahisi.
Katika mahojiano maalum na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ambaye
anaeleza mambo mbalimbali yaliyofanya Yanga kuwa imara zaidi msimu huu, lakini
pia walipofeli na kipi wamepanga kukifanya ili kuimarika zaidi.
Yanga ina tofauti kubwa na
miaka ya nyuma, sasa kuna utulivu na mshikamano. Je, nini siri ya hili?
Sanga: Kweli klabu kwa sasa
ina utulivu mkubwa kwa kuwa uongozi ni ule ulio tayari kupokea changamoto na
kuzifanyia kazi.
Lakini utaona, viongozi ni
wale wanaojituma na kutakiwa na wanachama. Yaani hawapo tayari kuharibu kwa
hofu watakosa nafasi ya uongozi, badala yake wanataka kufanya kile kilicho
sahihi.
Hii imesaidia kuwaunganisha
watu ambao nao wapo tayari kushirikiana nao.
Kuna marekebisho ya katiba,
nini faida yake?
Sanga: Yamekuwa na faida,
pia hasara zake. Lakini utaona sasa kuna watu maalum kwa ajili ya kufanya kazi
fulani, si kila mtu anaweza kufanya.
Hiyo inaipa klabu nguvu na
kazi kufanyika kwa mpangilio zaidi kwa kuwa klabu inaweka mambo wazi, yaende
vipi na hakuna utata.
Awali kila mmoja alikuwa
anataka afanye anavyotaka yeye. Lakini pia mabadiliko hayo pamoja na utendaji
wa uongozi wa juu, mimi na mwenyekiti wangu (Yusuf Manji) tunaendana kimawazo,
nini tunataka kufanya kwa manufaa ya klabu na hata tukipishana bado inakuwa ni
kwa faida ya klabu.
Kuifuata katiba, kunasaidia
kutokuwa na migogoro. Halafu uongozi wa juu unapoelewana, unasaidia kutoibuka
kwa migogoro pia.
Kuna shida kidogo, bado
kuna wale ambao wako katika kamati mbalimbali hasa wa kuteuliwa. Wanakuwa
hawana morali maana wana mambo yao mengi. Hapa ni lazima kuwe na mabadiliko kwa
kuwa kazi hii ni ya kujitolea.
Pamoja na majukumu yangu,
nimekuwa nikijitolea zaidi, lakini bado naona sijafanya vya kutosha kuisaidia
Yanga.
Sasa kuna umoja wa hali ya
juu kwa wazee na vijana kutaka kuisaidia klabu. Nini kimefanyika kuwashawishi
hadi wanajitolea kiasi cha juu kabisa?
Sanga: Kwanza tuliwaeleza
ukweli kwamba kikatiba hawatambuliki, lakini bado tukaendelea kuyaenzi makundi
haya. Hata kitaifa hakuna wazee wa Dar es Salaam. Lakini rais huwaita na
kuzungumza nao, wana umuhimu wao.
Hali kadhalika, uongozi
wetu ulilitambua hilo. Tumeendelea kuwaenzi, tunafanya nao kazi vizuri.
Tunachukua maoni yao na tunayafanyia kazi kwa niaba ya klabu.
Wachezaji wanaonekana kucheza
kwa ari kubwa, mmeweza kuwashawishi kwa kipi, mishahara mikubwa au kwa njia
zipi?
Sanga: Sisi ni binadamu,
huenda kuna makosa tunafanya. Lakini ukizungumzia kulipa, mara nyingi
tunajitahidi malipo yawe kwa wakati.
Tuko karibu na wachezaji na
benchi la ufundi na tunawapa nafasi ya kufanya kazi yao kitaalamu.
Mlimuondoa Marcio Maximo ikiwa
ni siku chache baada ya kumleta kutoka Brazil. Unafikiri mlikurupuka kumleta, pia
mkafanya hivyo kumuondoa?
Sanga: Kila kocha ana
falsafa yake, (Hans van Der) Pluijm ameonyesha ni kama mzazi, anajua namna ya
kukaa na wachezaji, anajua afanye nini kupandisha viwango vyao.
Kama unakumbuka tuliamua
kumleta Maximo baada ya kuondoka kwa Pluijm ambaye alipata ofa kubwa sana Saudi
Arabia. Tusingeweza kumzuia yeye na (Boniface) Mkwasa, nao ni binadamu na
wanatafuta maisha.
Tulimleta Maximo ingawa
kweli tulipata ushauri kwa baadhi ya watu wakieleza matatizo yake. Lakini bado
tuliamini atatusaidia, kama unakumbuka Taifa Stars yake ilifanya vema kiasi
fulani.
Lakini kufanya naye kazi ilikuwa
ni kazi ngumu, hapokei ushauri, anaamini anajua zaidi na yeye ni kocha mkubwa.
Ikatushinda, tuliamua kumrudisha Pluijm.
Utaona, anafanya kazi vizuri.
Wachezaji kama Msuva sasa wamepanda tena viwango baada ya kuwakuta wameporomoka
kabisa.
Amejenga timu kwa muda
kidogo, utaona tulishinda mbili, tatu. Sasa ni hadi tano au nane. Kikosi
kinakwenda kinaimarika.
Mnafanya vizuri michuano ya
kimataifa na nyumbani, sasa mnakutana na Etoile du Sahel ya Tunisia. Hawa ni
Waarabu, mnalitambua hilo?
Sanga: Tunalitambua hilo,
Yanga ya sasa imebadilika, hata wachezaji wanajua wanataka nini. Wanataka
wafanye kitu kipi, mshikamano na wanachama na mashabiki uko juu.
Ndiyo maana Yanga imepoteza
dhidi ya Simba, siku chache watu wamesahau kwa kuwa wanajua wanataka nini.
Maandalizi yameanza,
tunaweza hata kuwahi Tunisia. Msimu uliopita Yanga iliifunga Al Ahly Dar es
Salaam, tukatolewa kwa penalti kule Alexandria, Misri. Tulivunja mwiko wa
kutowafunga Waarabu hasa wa Misri. Tunataka kuendeleza zaidi ya hapo.
Mnajitahidi kufanya mazuri,
lakini Simba inaonekana kuwashinda kabisa, kwa nini?
Sanga: Naamini uongozi wetu
hauko madarakani kuifunga tu Simba. Kwanza ni kuchukua ubingwa. Ingekuwa lengo
ni kuwashinda Simba pekee, tusingekuwa hapa leo. Lakini tunaendelea kujiweka
sawa, siku tutafanikiwa.
Unafikiri uongozi wa juu wa
TFF kuwa na Yanga wengi inawasaidia?
Sanga: Yamekuwa ni mawazo
ya wengi, kwanza tunakubali TFF ina Yanga wengi. Lakini kwetu tunaona ndiyo
inatuumiza zaidi, huenda wanahofia kutenda haki kwa kuonekana Yanga. Angalia
suala la kadi tatu za njano za Ibrahim Ajibu wa Simba, liko wazi ni tatizo
lakini TFF imeshindwa kuchukua hatua.
Yanga inahusika katika
historia ya uchumi wa nchi hii. Tena kupitia CCM, sasa kabla hawajachagua
mgombea, mnamuunga mkono nani?
Sanga: Hatutaingia katika
kundi lolote, hatumuungi mkono mwanachama yeyote wa CCM, Chadema au chama
kingine chochote. Wala hatutajiingiza kwenye kampeni za wagombea.
Ila tunaweza kufanya mambo
ya kijamii, mfano kuhimiza watu wapige kura. Watu wawe makini kuepusha vurugu
na kuipoteza amani yetu na si vinginevyo.
Naona kama unakimbia
kuingia ndani ya CCM, wakati hata mkishinda, mashabiki wenu huimba “CCM, CCM”
Sanga: Nafikiri ni
historia, pia ishu ya rangi za njano na kijani. Lakini unaweza kuwa CCM ukawa Simba.
Mfano mzuri ni Profesa Philemon Sarungi, Juma Kapuya au Ismail Aden Rage na
wengine wengi.
Inaonekana kujenga uwanja
kumewashinda kabisa, ni kweli?
Sanga: Tuna maombi yetu ya
kuongezewa sehemu tuliyapeleka serikalini. Hadi sasa tunaendelea kusubiri na
hilo ndilo linalotukwamisha.
SANGA ANA AKILI SANA.
ReplyDelete