Kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
ambaye hajawahi kuipenda Yanga hata kwa utani, ameibuka na kuipa timu hiyo
mbinu za kuiua Etoile du Sahel ya Tunisia katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.
Julio alisisitiza kuwa, ili waweze kufanikiwa
kuwaondoa Waarabu hao, wanatakiwa kwenda kwa tahadhari na kuepuka fitna zao.
Yanga inatarajia kurudiana na Etoile kati ya
Mei Mosi hadi tatu nchini Tunisia, baada ya mchezo ule wa awali kutoka sare ya
bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar, hivyo inalazimika kupata sare ya zaidi ya
bao moja au ushindi ili kusonga mbele.
Julio
amesema kuwa Yanga ina kibarua kigumu cha kuhakikisha inafanikiwa kuwaondoa
wapinzani wao katika michuano hiyo na kudai kuwa Waarabu wana fitna sana, hasa
wanapokuwa nyumbani kwao.
“Yanga wanatakiwa kwenda kucheza kwa tahadhari
kubwa ili waweze kushinda katika mchezo wa marudiano kwa kuwa Waarabu ni watu
wenye fitna sana.
“Mchezo wa marudiano utakuwa mgumu, hivyo
wanahitaji kujipanga na kutathmini mchezo uliopita na kuhakikisha wanafanya
vyema katika mchezo unaofuata, naamini hakuna kitakachoshindikana iwapo
kutakuwa na mipango madhubuti,” alisema Julio.
0 COMMENTS:
Post a Comment