Klabu ya Simba sasa imeamka na kuisogelea nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, lakini habari ni kuwa imeshinda mabao saba katika michezo miwili mfululizo bila ya kuwa na ‘orijino’ straika katika kikosi chake.
Simba sasa inashika nafasi ya tatu katika
msimamo wa ligi ikiwa na pointi 41, huku Yanga wakiendelea kutesa kileleni na
pointi 52 wakifuatiwa na Azam FC wenye 45.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumatano
iliyopita, Simba ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Mgambo JKT kabla ya juzi Jumamosi
kuifunga Ndanda FC mabao 3-0, michezo yote ikipigwa kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar.
Katika michezo hiyo, kuanzia namba sita mpaka
11 Simba iliwatumia viungo wakabaji na viungo washambuliaji, lakini bado ilifanikiwa
kuwatesa wapinzani wake, tena kwa idadi kubwa ya mabao.
Simba iliwatumia Said Ndemla, Jonas Mkude,
Awadh Juma, Emmanuel Okwi, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Ibrahim Ajibu ambao
kiuhalisia hakuna hata mmoja ambaye ni mshambuliaji wa kati.
Okwi na Ajibu walikuwa wakibadilishana nafasi
ya kucheza ‘sentro straika’ kulingana na mazingira ya mchezo husika
yalivyokuwa, ambapo wachezaji hao wote wana uwezo wa kucheza nafasi hizo wakiwa
uwanjani.
Mabao hayo saba katika michezo hiyo miwili
yalifungwa na Okwi aliyetupia matatu, Singano alifunga mawili, huku Mkude na
Ndemla kila mmoja akifunga bao moja.
Wachezaji wa Simba ambao ni orijino straika ni
Elias Maguri na Mganda Dan Sserunkuma ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza
mara kwa mara katika kikosi hicho kinachonolewa na Mserbia, Goran Kopunovic
ambaye amejiunga na kikosi hicho siku 117 zilizopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment