Katika kuhakikisha wanakuwa na kikosi
bora zaidi msimu ujao, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amependekeza
wasajiliwe wachezaji wanne kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chake.
Yanga imekuwa ikimtumia Amissi Tambwe
kama mshambuliaji wa kati ambapo hana msaidizi hadi sasa iwapo atapata majeraha
kutokana na Kpah Sherman kutokuwa fiti.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga kimeeleza wapo katika mikakati ya kusaka
wachezaji wanne kwa ajili ya usajili wa msimu ujao ili kuimarisha kikosi hicho
kwa ajili ya ligi na michuano ya kimataifa.
Nafasi ambazo zinatarajiwa kuzibwa
katika usajili wa msimu ujao ni pamoja na walinzi wa pembeni, kiungo,
washambuliaji wa kati na viungo wa pembeni ili kuweza kuimarisha kikosi.
“Tunahitaji kukiboresha zaidi kikosi msimu
ujao kwani kumekuwa na upungufu mkubwa katika safu ya ushambuliaji, jambo
ambalo uongozi umekutana na kocha ambaye ametaka nafasi hizo zifanyiwe kazi.
“Mchakato bado unaendelea na tumepanga
kuongeza wachezaji katika nafasi nne ambapo suala la ushambuliaji ndilo
limekuwa tatizo zaidi.
“Kwa sasa tunatafuta viungo wa pembeni
pamoja na wa kati ili kuja kusaidiana na Tambwe, tunaamini tukileta mchezaji
mwenye uwezo mzuri Tambwe atakuwa huru zaidi.
“Nafasi nyingine ni pamoja na walinzi
wa pembeni na viungo ambao tunaamini wataimarisha timu, kwa sasa bado
tunaendelea kuangalia wachezaji kutoka timu mbalimbali za ligi kuu,” kilisema
chanzo hicho.
0 COMMENTS:
Post a Comment