Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mrundi,
Amissi Tambwe, ameitupia dongo kiaina timu yake ya zamani ya Simba akisema
anashukuru kwa kuwa yupo Yanga ambako ana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
Bara lakini kama angeendelea kukaa Msimbazi, asingepata nafasi hiyo.
Msimu uliopita, Tambwe alikuwa Simba na
kuibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 19 lakini alishindwa kupata ubingwa
huo, baada ya timu yake kushika nafasi ya nne.
Yanga sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 52
na kama leo itafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo dhidi ya Polisi Moro
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, itakuwa tayari imeubeba ubingwa huo
unaoshikiliwa na Azam FC.
Akizungumzia kuchukua ubingwa wa kwanza wa
ligi kuu, Tambwe amesema atafurahia kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza
akiwa na Yanga baada ya kushindwa kufanya hivyo akiwa Simba, ingawa alidumu
klabuni hapo kwa muda mrefu.
“Ninamshukuru Mungu msimu huu kwa kuwa nitafanikiwa
kuchukua ubingwa nikiwa na Yanga, ni jambo la faraja sana kwangu kwa sababu
nilifeli nikiwa Simba, ingawa nilikaa kwa msimu mzima, lakini hapa Yanga nina
muda mchache tu tangu nijiunge nao.
“Hii ni historia nzuri kwangu na inanifanya
niwe na faraja kwa sababu kila mchezaji anapambana ili kupata mafanikio,
ikiwemo mataji, ndiyo maana ninajituma sana uwanjani, kama nisipofunga basi
nitoe pasi ya bao,” alisema Tambwe ambaye mpaka sasa ameifungia Yanga mabao 11
katika Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment