April 20, 2015


Kiungo wa Yanga, Mnyarwanda, Mbuyu Twite, juzi aliweka rekodi ya pekee kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika walipovaana na Etoile du Sahel.


Twite ameweka rekodi ambayo ni adimu sana kuiona hata barani Ulaya, baada ya kutumia dakika tisini kucheza nafasi tatu uwanjani.

Kiungo huyo ambaye anamaliza mkataba wake na Yanga mwishoni mwa msimu huu, alianza mchezo wa juzi akiwa kama kiungo namba sita, lakini baada ya kipindi cha pili kuanzia, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliumia na kutoka na nafasi yake kuchukuliwa na Saidi Juma Makapu, ambapo ilimlazima Twite kucheza namba tano na Makapu namba sita.

Hata hivyo, muda mchache baada ya mabadiliko hayo, Etoile walipata bao ambalo liliwafanya wapate sare ya bao 1-1 kwenye mchezo huo.

Huku dakika zikizidi kwenda, beki namba mbili wa Yanga, Juma Abdul, naye aliumia na kutoka nje ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Rajab Zahir, ambaye ilibidi aingie na kucheza namba tano na Twite kwenda kucheza kwenye nafasi ya Abdul.

Jambo la ajabu ni kwamba kwenye nafasi zote ambazo kiungo huyo wa zamani wa APR ya Rwanda alicheza, alikuwa akionyesha kiwango cha hali ya juu kilichowashangaza mashabiki waliokuwa wamejazana uwanjani hapo.

Imekuwa ikielezwa kuwa Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amekuwa akisema kuwa lazima watambakiza mchezaji huyo hata baada ya mkataba wake kumalizika kutokana na kuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani, yaani kiraka.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic