![]() |
| OKWI WAKATI AKIKIPIGA ETOILE... |
Wakati
wewe ulifikiri Etoile du Sahel wana mpango wa kulipa zile dola 300,000 (Sh
milioni 480), wenyewe walikuwa jijini Dar es Salaam wakisaidiana na Shirikisho
la Soka la Tunisia (FTF) wakitaka kumpata Emmanuel Okwi.
Makamu
wa Rais wa FTF, Krifa Jalel, amesema walimsaka Okwi bila mafanikio ili
wazungumze naye na kujua sababu ya kutoroka kazini.
Jalel
amesema waliomba waletewe Okwi bila ya mafanikio na walishirikiana na Rais wa
Etoile du Sahel (ESS), Charefeddine Ridha aliyekuwa jijini Dar es Salaam
kumpata Okwi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, juzi, Jalel alisema anashangazwa na
kuona Simba wanadai fedha wakati Okwi sasa anaichezea Simba.
“Sasa
wanataka walipwe fedha za nini? Okwi si yuko hapa anaichezea Simba? Tumetaka
kukutana naye ili tuzungumze na kutatua tatizo lake, hakuna aliyetusaidia
kumpata.
“Nilizungumza
na baadhi ya viongozi wamlete, hakuna aliyetusaidia. Nilitaka kumuuliza kwa
nini aliondoka Tunisia baada ya miezi sita na hakurejea,” alisema na
alipoulizwa kama ni viongozi wa Simba ambao hawakuwapa msaada alisisitiza:
“Wewe
jua ni viongozi tena wahusika. Sasa sioni kama kuna sababu ya kulipa ingawa
bado Etoile ndiyo watalitolea uamuzi.”
Alipofuatwa
kiongozi mwingine wa Etoile, yeye alisema suala la Okwi liliisha na hawana
sababu ya kulizungumzia kwa kuwa yupo Dar es Salaam walipomtoa na anaichezea
timu yake ya zamani, hivyo hakuna kilichoharibika.
“Nafikiri
unataka kunitega sijui niseme nini. Okwi yupo hapa kwenu anaichezea timu yake.
Sasa tulipe kwa kuwa anaichezea Simba! Si tayari Simba wana mchezaji wao,”
alihoji.
Etoile
iliahidi kulipa fedha hizo kwa ajili ya Okwi baada ya Simba kukubali kumuuza ‘bure’
kupitia aliyekuwa mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage.
Lakini
Simba imesema tayari Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeagiza Simba
ilipwe fedha hizo lakini Etoile wamekuwa wakisuasua na kauli walizozitoa katika
mahojiano hayo juzi, zinaonyesha huenda fedha hizo kulipwa, itakuwa ndoto kama
Simba wasiposimama kidete.
SOURCE: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment