UTATA
kuhusiana na kundi la mashabiki na wanachama wa Simba kutoka Tawi la Mpira
Maendeleo maarufu kama Simba Ukawa umekuwa mkubwa sana, unakumbuka wakati
fulani hadi mashabiki wengine walitaka kuwapiga.
Askari
Polisi wakafanya kazi ya ziada kuwatoa uwanjani kwa usalama. Basi lao
likasindikizwa na kweli wakafanikiwa kutoka kwa usalama.
Mechi
iliyofuata, Simba Ukawa walikuwa uwanjani kwa mara nyingine wakiendelea
kuishangilia timu yao kwa nguvu zote bila ya woga.
Kumekuwa
na taarifa kadhaa ambazo zinaelezwa kuhusiana na Simba Ukawa. Unakumbuka kile
kipindi cha sare sita mfululizo? Ilielezwa Ukawa walikwenda kwa “Babu” ili
Simba wapate sare saba mfululizo bila ya kushinda.
Hali
ile na namna ilivyokuwa ikisambazwa ilisababisha chuki kali baina ya Simba
Ukawa dhidi ya mashabiki wengine wa Simba baada ya kuona wenzao wakiwahujumu.
Bado
yote hayakuwa na uhakika lakini Ukawa wamekuwa wakisisitiza kuwa lengo lao ni
kuishabikia Simba na furaha yao ni kuona inaibuka na ushindi ukiachana na
maneno mengine ambayo yamekuwa yakielezwa na watu.
Bahati
mbaya imetokea siku chache zilizopita baada ya mashabiki sita wa Simba Ukawa
kupoteza maisha wakati wakiwa njiani kwenda kuishangilia Simba iliyokuwa
ikipambana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Baadaye
mechi ile iliahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, sasa inachezwa leo.
Ajali
hiyo iliyotokea mkoani Morogoro, imewachukua mashabiki hao sita pamoja na watu
wengine watatu ambao walielezwa kuwa ni abiria waliopanda katika basi lile
lililoteleza na kuacha njia. Ni huzuni kubwa kwa wapenda michezo na hasa soka.
Kwangu
nawachukulia Ukawa waliopoteza maisha au kuumia kuwa ni mashujaa wa klabu ya
Simba na wanastahili kuthaminiwa sana na uongozi wa klabu hiyo.
Hao
walikuwa ni mashabiki na wanachama ambao waliamua kujitolea mambo mawili
makubwa ambayo mwanadamu anaweza kuwa mgumu sana kuyatoa kwa mtu au kitu
asichokuwa na mapenzi nacho.
Yanapaswa
kuwa mapenzi tena ya dhati kwa mwanadamu kutoa muda wake au fedha zake. Ukawa
walifanya hivyo kwa Simba, maana walikubali kuchangisha fedha zao ili
wakaishangilie Simba.
Walitaka
kuipa nguvu ili iitwange Kagera. Walitoa pia muda wao ambao wangeweza kuutumia
kutafuta fedha au kuzihudumia familia zao na kama ni mechi tu basi wangeweza
kuishuhudia kupitia Azam TV, kusikiliza kwenye rekodi au kusoma matokeo katika
Championi kwa kuwa wanajua ni gazeti la uhakika.
Lakini
wakaamua kusafiri wakijua safari ni hatua, tena ni safari ndefu ya zaidi ya saa
12 wakiwa wanahangaika njiani. Ili mradi tu kuisaidia Simba ili ifanye vema.
Ndiyo starehe yao, timu hiyo ndiyo amani ya mioyo yao. Lakini Mungu anapanga
yake na siku zote ndiye aliye sahihi.
Vifo
vyao vinauma kwa wana ndugu na rafiki zao lakini vinapaswa kutuumiza hata
wanamichezo na wadau wa mchezo wa soka. Viongozi wa klabu ya Simba pia
wanapaswa kuguswa na maumivu yao.
Nimesikia
wametoa rambirambi. Linaweza kuwa jambo zuri sana, lakini lazima wajue
majemedari wao waliopoteza maisha wakiwa njiani kwenda kuipigania Simba, wana
familia. Mfano wazazi, watoto, wake au waume, ndugu na jamaa.
Wanaweza
kufanya jambo. Kwangu siamini rambirambi pekee kama fedha inatosha. Kama
hawakufanikiwa kufika katika mazishi, basi Simba ina viongozi wengi. Wanaweza
kufika nyumbani kwa wahusika na kuzungumza na familia zao.
Sijasema
wasomeshe watoto wao, sijasema wahudumie familia zao maana sijui uwezo wa klabu
hiyo na viongozi wake. Lakini bado wana uwezo wa kuonyesha upendo zaidi ya hapo
na ikiwezekana sasa ndiyo uwe mwisho wa tofauti za Simba Ukawa na Simba.
Mwenyezi
Mungu ana yake mengi. Huenda pia alichoshwa na kelele za sehemu hizo mbili.
Raha na matatizo huwa ni sehemu mbili za kutatua matatizo yanayowakabiri. Simba
wanaweza kutatua matatizo yao sasa na kurejesha upendo uwaongoze.
Mungu azipumzishe kwa
amani, roho za waliotangulia mbele ya haki.
0 COMMENTS:
Post a Comment