Na Saleh Ally
MWISHO ilikuwa mwaka 2012 baada ya
Simba kuonja utamu wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, baada ya hapo imekuwa ni sawa
na hadithi tu.
Taji la mwaka 2012 lilikuwa na
kumbukumbu ya aina yake kwa kuwa Simba ilibeba ubingwa baada ya kuwaadhibu
watani wake Yanga kwa kichapo cha kukumbukwa. Simba ilishinda kwa mabao 5-0
katika mechi ya mwisho ya ligi.
Baada ya hapo, Simba imefanikiwa
kujipoza na makombe ya michuano mifupi kama Kombe la Mapinduzi, ubingwa wa
mechi ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe na kadhalika.
Hata iwe vipi, Simba inastahili
ubingwa. Hilo ni lazima na hakuna anayeweza kupinga kwa kuwa ni klabu kubwa na
historia yake inaweza ikawa inawahukumu kwa kuwadai ubingwa.
Miaka mitatu sasa, msimu huu bado Simba
haina uhakika wa kubeba ubingwa wa Tanzania Bara. Yanga wana asilimia 90 ya
kubwa mabingwa, Azam FC 78% na Simba 46%.
Bila shaka Simba haiwezi kuwa bingwa,
lakini katika nafasi ya pili, Azam FC ina 93% ya kuishika nafasi hiyo na Simba
79%.
Inaonekana hata nafasi ya pili kwa
msimu wa tatu kwenda wa nne ni uhakika Simba haiwezi kushinda nafasi zote mbili
za juu ambazo Yanga na Azam wamekuwa wakizitawala.
Miaka mitatu yote, Yanga imebeba
ubingwa mara mbili na Azam mara moja. Simba imeendelea kuambulia patupu na
nafasi zake ni ya tatu hadi tano, inatia huzuni.
Kinachoonekana Simba haiko vizuri,
baada ya timu yake ya msimu wa 2011-12 kuvurugika, kuanzia hapo imeanza kuyumba
na hakukuwa na mipango dhabiti ya kuitengeneza upya.
Wachezaji takribani sita wa kikosi cha
kwanza wakiwemo Kelvin Yondani, Emmanuel Okwi na wengine wengi waliondoka na
hawakupata warithi sahihi, japokuwa Okwi amerejea sasa.
Simba iliamua kujipanga kwa kutumia
vijana zaidi. Imewalea na kuwakuza wengi, baadhi yao kama Jonas Mkude,
Ramadhani Singano ‘Messi’, Hassan Isihaka sasa ni tegemeo.
Hali kadhalika Ibrahim Ajibu, Said
Ndemla na wengine wengi sasa wamekuwa tegemeo kwa Simba na wanapambana
kuisaidia timu. Ni jambo zuri.
Pamoja na mazuri ya vijana hao, huu ni
wakati mwingine mwafaka, Simba inapaswa ibadilike na kuamini sasa inatosha kuendelea
kusajili wachezaji wengi kwa ajili ya kujifunza.
Simba inahitaji wachezaji hasa ambao
wana uwezo wa kucheza. Haina maana wawatupe wachezaji vijana. Utaona imetumia
chipukizi wengi zaidi kwa miaka mitatu sasa na jibu liko wazi, hawawezi kubeba
kombe.
Makocha wawili walikuwa wazi na kusema
Simba haiwezi kubeba ubingwa kwa kikosi cha watoto wengi. Kocha Milovan
Cirkovic ndiye aliyekuwa wa mwisho mwenye kikosi imara zaidi, alipotua Patrick
Liewig ‘akatiwa ndimu’ kuhusu vijana, akawatupa wakongwe wote.
Ujio wa Zdravko Logarusic ulikuwa na
mabadiliko kwa kuwa alikuwa mkweli zaidi na kueleza si rahisi kubeba kombe na
watoto. Alionekana hakuwa sahihi na ana tabia ya kikorofi.
Patrick Phiri raia wa Zambia ambaye
amewahi kuinoa Simba na kuipa mafanikio makubwa naye alilisema hilo la vijana.
Kwamba timu yake ina watoto na vijana wengi, hivyo si rahisi kuzungumzia
ubingwa.
Kama Simba wanataka ubingwa, basi suala
la kujaza vijana wengi kwa madai wanawakuza, sasa basi imetosha. Vijana
waliowakuza kama akina Ndemla, Mkude na wengine wanawatosha.
Wanaweza kuendelea kuwakuza wengine kwa
kuwaingiza wachache katika kikosi kikubwa na wengi vijana wakabaki katika
kikosi cha vijana lakini si vijana wengi kuwa katika kikosi kikubwa, hakika
Simba haitafanikiwa.
Kama Simba inataka kuwa timu ya kuwania
ubingwa, bado ina nafasi iwatumie vijana ilionao sasa kwani tayari wameanza
kukomaa. Halafu iongeze angalau wachezaji 10 wa uhakika. Mfano wageni watano,
pia wachezaji wa nyumbani watano.
Suala la kukuza vipaji ni zuri na la uhakika
lakini Simba lazima ikubali kuwa inatakiwa kuchagua. Kuendelea kukuza vijana au
kugombea kutwaa ubingwa.







Simba waache kusingizia kukuza vipaji wakati kila wakikutana na yanga wanaifunga,sasa kwanini wasiwafunge na Mbeya city?Mipira ya kishirikina ndio tatizo la simba hawachezi kwa ufundi uwanjani zaidi ya kuroga tuu.
ReplyDeleteSimba ina wachezaji wakigeni watano,pia ina Ivo mapunda,cholo,Baba ubaya na wengine kadhaa wote ni watu wazima kumkaribia Saleh Ally,sasa utoto wao ukowapi?
Mwandishi wa makala hii naye anaegemea kulekule eti wanakuza vipaji,huu sasa ni mwaka watatu hivyo vipaji havikui tuu/
Acheni longolongo chezeni mpira.