MASHABIKI wa Yanga kutoka katika kundi
linalojulikana kama Yanga Facebook Family, wamejitokeza na kutoa tuzo kwa
kikosi kizima cha Yanga.
Zawadi hizo zilikabidhiwa juzi kwenye Uwanja
wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam wakati Yanga ikiendelea na maandalizi yao
kujiandaa na mechi ya leo dhidi ya Mbeya City.
Uamuzi wa mashabiki hao ambao sasa taratibu
wanakua na huenda wakawa taasisi inayotambulika unaonyesha kiasi gani mapenzi ya
dhati yanavyoweza kupita katika njia sahihi.
Walichofanya ni kutoa tuzo kwa kikosi kizima
cha Yanga wakianza na wachezaji, mtunza vifaa, mchua misuri, daktari, meneja,
kocha msaidizi na kocha mkuu.
Zawadi walizotoa ukiziangalia unaweza
kudharau, lakini hakika wanaonyesha ni watu waliojipanga na walikusudia kufanya
jambo kwa ufasaha kabisa.
Walitoa flemu maalum zilizoandikwa majina ya
wahusika kukiwa na picha zao, walitoa vinyago hii wakionyesha kudumisha thamani
ya utamaduni wa Mwafrika.
Pia walitoa picha maalum, kubwa zenye ujumbe
unaoonyesha kuthamini kazi ya mchezaji husika ikiwa ni sehemu ya morali
kukitaka kikosi chao kiendelee kupambana vilivyo kwa kuwa kazi bado.
Sijuo Yanga Facebook Family wanaendesha
mambo yao namna gani. Lakini ni watu ambao wameonyesha mabadiliko makubwa kwa
kuwa safari hii mashabiki ambao wako karibu na timu wamekubali kutoa chao
mfukoni ili kuipa timu morali.
Huenda wako wachache waliwahi kufanya hivyo
huko nyuma, hongera zao. Lakini leo Yanga Facebook Family ndiyo wanastahili
pongezi kwa kuwa wameonyesha unaweza kuipenda Yanga bila kupata chochote
unachoweza kuingiza mfukoni.
Mashabiki wengi wa Yanga au wanachama
nimekuwa nikipambana nao kuwaeleza ukweli kuhusiana na suala la mapenzi feki
kwa klabu zao, wanajidai wanazipenda kumbe ndiyo sehemu yao ya kuchumia riziki.
Wako wale ambao ni wapambe wa baadhi ya
viongozi wa klabu hizo. Wanajua watapata chochote kila watakapomuona kiongozi
wa klabu. Wanasingizia mapenzi, kumbe ni ahueni ya njaa zao.
Wako ambao wamekuwa wakigombana na viongozi
wanaopeleka mambo yakiwa yamenyooka. Lakini wanawachukia kwa kuwa tu hawawapi
fedha au ‘hawawapozi’ ili wapate kupunguza ukali wa maisha.
Mashabiki au wanachama hao wako tayari hata
kumuumiza mtu wakisingizia eti wanaipenda sana Yanga. Wanafanya hivyo kwa kuwa
Yanga ni mtaji wao wa kujipatia riziki.
Najua mmekuwa mkikasirika sana kueleza
ukweli. Mimi natumia nafasi hii kuwakasirisha tena kwa kuwakumbusha kuwa Yanga
Facebook Family wamewaumbua na wanaonyesha unaweza kuipenda Yanga bila ya kuwa
katika kundi la Makomandoo wenye jeshi feki.
Wanachama na mashabiki hao wamekuwa
wakisababisha chokochoko mara kwa mara ndani ya klabu ya Yanga kwa kuwa tu
hawakupewa fedha, hawakupewa nafasi ya kukaa milangoni au vinginevyo.
Wamekuwa wakianzisha vita na waandishi bila
ya sababu za msingi, kisa eti bosi fulani kasemwa vibaya. Ukiulizwa utaambiwa
ndiye ambaye amekuwa ‘akiwapoza’, hivyo wanataka kumuonyesha hasira na machungu
yao kwake, ili awapoze zaidi.
Usipokuwa makini, utaona kweli ni watu
wanaoipenda klabu hiyo, kumbe ni wale wanaothamini matumbo yao na mapenzi yao
kwa klabu ni kunufaisha nafsi zao. Hii ipo hata kwa jirani au watani wao Simba
ambao pia wana hao wanaoamini wao ni makomandoo ambao kwangu nimekuwa nikiamini
ni feki na hawana msaada wowote katika klabu hizo mbili kongwe.
Kundi la Facebook Family, walisafiri kwa
wingi hadi Zimbabwe kupambana kuhakikisha Yanga inasonga mbele. Kweli imekuwa
hivyo.
Sasa wametoa zawadi, ambayo ni motisha ya
juu, ikiwezekana hata uongozi au wadhamini wa klabu hiyo hawakuwahi kufanya.
Ukiangalia vitu walivyotoa, kwangu nakadiria
haiwezi kuwa chini ya milioni nne tano. Sasa hauoni hawa watu wanaipenda klabu
yao? Vipi wewe unayetaka klabu ndiyo ikupe fedha, acheni kabisa. Iko siku
nitawataja kwa majina, mmoja baada ya mwingine. Subirini tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment