Na Saleh Ally
UJIO wa Klabu ya Azam FC umekuwa ukizungumzwa
kama sehemu ya mapinduzi ya mchezo wa soka nchini.
Kwamba ndiyo wakati mwafaka wa kuhakikisha mabadiliko
yanapatikana na kuachana na mengi yaliyotufelisha huko tulikopita. Unaweza
kusema ndiyo kwa kuwa walianza kuonyesha mfano.
Azam FC wamejenga sehemu nzuri kwa ajili ya
kukuza vipaji na wana uwanja wao ambao ni kati ya viwanja vinavyotumiwa katika
Ligi Kuu Bara.
Ndani ya misimu minne, tayari Azam FC
wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara. Lakini walifanikiwa kushika
nafasi ya pili mara mbili.
Utaona ni kikosi kilicho na mwendo mzuri na wa
kuvutia. Lakini baada ya hapo, yakaanza kuingia mambo mengi ya “Kiswahili”.
Haikuwa rahisi viongozi wa Azam FC kukubali
kwamba kuna mambo hayafai yamekuwa yakiingia ndani ya klabu hiyo, huenda
kutokana na suala la kimaslahi.
Kunapokuwa na maslahi kawaida fitna haikosekani, huo ndiyo
ulikuwa mwanzo wa Azam FC kuwa na maneno mengi ya chinichini.
Huenda hii ilikuwa na tofauti kubwa
ukilinganisha na wamiliki wake walikuwa wanataka nini hasa katika maendeleo ya
klabu hiyo.
Sifa moja ya Azam FC wakati ikipanda lilikuwa
ni suala la maendeleo na kwenda mwendo tofauti na wakongwe wa soka nchini.
Huenda wapo wengi walioitumia Azam FC kama fimbo kuzichapa Yanga na Simba.
Lakini sasa mbona ndani ya klabu hiyo changa ni yaleyale kama ya Simba?
Tunajua kumekuwa kuna hali ya kutoelewana kati
ya viongozi na wachezaji au wachezaji na viongozi. Hilo likizungumzwa kwa kuwa
Azam FC wamekuwa wakijiona ni bora, wasiotakiwa kuambiwa na kila wanachoambiwa
wanaona wanapigwa vita, mambo yamekuwa yakijificha.
Mficha maradhi, kifo humuumbua. Juzijuzi
viongozi wa Azam FC wametaka kuzichapa hadharani, tena mbele ya kundi la watu
wengi. Sasa hii si siri tena!
Swali langu la kwanza, tuache kuzungumzia kwa
kuwa Azam FC watasema hatuwapendi au wanasakamwa? Kwani Azam FC ni nani hasa
wasiambiwe ukweli, eti watanuna? Wanune lakini ukweli unaanza leo.
Kwamba wapo watu wawe viongozi au wengineo
wanaingiza maisha yao ya mfumo uleule wa Yanga na Simba uliokuwa ukionekana
haufai. Ndiyo maana si rahisi wao kusikilizana.
Waliotaka kupigana hadharani ni meneja wa
timu, Jemedari Said dhidi ya bosi wake, Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba.
Juhudi za baadhi ya viongozi wengine akiwemo
Iddi Cheche kama unavyoona kwenye picha ndizo zilisaidia kuzuia wawili hao
kutotandikana ngumi kwa kuwa kila mmoja alikuwa tayari.
Fedheha ya kutaka kupigana mbele ya watu, tena
kwenye Uwanja wa Chamazi ambako ni nyumbani kwao haileti picha nzuri. Acha
hivyo, iweje hata kama wamepishana kauli walishindwa kutembea hatua 20 au 30
kuingia kwenye vyumba au ofisi zao na kulijadili hilo?
Jemedari amecheza soka, anajua namna wachezaji
wanavyoweza kumuamini na kujivunia kiongozi wao ambaye ana uwezo wa kufanya
maamuzi, busara pia katika uongozi.
Kawemba alikuwa TFF, mama wa soka Tanzania.
Leo anaonekana anataka kupigana hadharani kwa kuwa amri yake haikuweza
kutekelezwa, hili ni sawa?
Bado naamini wao ni binadamu kama walivyosema,
lakini walikuwa Chamazi, sehemu ambayo ilikuwa rahisi kwao kukaa na kuzungumza
au kuondoka katika macho ya watu na kuzungumza pamoja kuhusiana na hilo.
Kitendo cha viongozi hao wa juu katika kikosi cha
Azam FC kutaka kupigana hadharani, kinaanza kutoa majibu kuwa kuna mambo ambayo
si sahihi yanaendelea chinichini.
Azam FC wamekuwa wakijitahidi kuyaficha kutaka
kuonyesha hawapendwi au vinginevyo, lakini mara kadhaa nimekuwa nikisema wazi
wanataka kujikweza waonekane kama Yanga au Simba, lakini si sahihi kwa kuwa
bado wanahitaji muda.
Kwangu Jemedari ni mtu mwelewa na amekuwa
akitoa ushirikiano kwa wanahabari. Sijui jibu alilopewa ni nini hadi kufikia
kutaka kupigana na Kawemba. Lakini lazima akubali, kwamba kuna tatizo na
hawawezi kutaka kupigana kwa tatizo la siku moja tu.
Zengwe ni sumu ya soka hapa nyumbani, ingawa
wapo wanaoamini mambo hayaendi bila ya zengwe. Azam FC hata kama imepata
mafanikio ya haraka kwa kuwa wamiliki wana fedha nyingi, lazima ikubali kuna
mengi inastahili kujifunza.
Wakati inajifunza, basi ipite njia ya
kuyafanya mabaya ya Yanga na Simba ni somo kwao badala ya kurudi na kuanza
kupita mulemule halafu waamini kuwa wao ni bora.
Kawemba aliyetoka TFF, anapaswa kuwa mfano. Hata
kama anatoa maagizo kwa watu wake lazima akubali kutumia njia nzuri badala ya
ukiwa bosi, kutaka kujifanya “Mungu”.
TFF ni kati ya taasisi kubwa zilizofeli kwa
miaka nenda rudi, hata kabla ya kuingia kwa Leodegar Tenga hadi leo akiwepo
Jamal Malinzi. Sasa kuna kila sababu ya Kawemba kuonyesha yuko Azam FC
kuisukuma mbele na si kuingiza ‘damu’ ya TFF ambayo majibu yake ni kufeli.
0 COMMENTS:
Post a Comment