KIUNGO mwenye kasi wa Yanga, Simon Happygod Msuva ameondoka
nchini kwenda katika Klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa ajili ya
kufanya majaribio.
Rasmi Msuva ameanza majaribio jana katika timu hiyo
inayomilikiwa na kitengo cha michezo cha moja ya vyuo vikuu vikongwe kabisa
barani Afrika cha Wits.
Chuo hicho kipo katikati kabisa ya Jiji la Johannesburg,
sehemu inayojulikana kama Sturrock Park.
Msuva ana hamu ya mafanikio, tumeona juhudi zake zilivyo na
wakati Yanga inachukua ubingwa, tayari ndiye kinara wa washambuliaji waliofunga
mabao mengi baada ya kuwa ametupia mabao 17.
Anakwenda kufanya majaribio akiwa mmoja wa wachezaji tegemeo
katika kikosi cha Yanga na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Wakati anakwenda kufanya majaribio, lazima Msuva awe mtu
anayejitambua kwamba sifa au kiwango chake ni kipi na anastahili kupata huduma
ipi au ya namna gani.
Nani anayemsimamia Msuva katika suala hilo? Kama ni wakala
au meneja. Je, yeye amelenga kupata nini hasa? Nia au lengo lake ni lile sawa
na anachotaka kiungo huyo mwenye kasi au kila mmoja ana lake analolitaka?
Wakala wa Zlatan Ibrahimović alimkataza mchezaji wake
kufanya majaribio Arsenal. Baada ya kuwa wamefika, Kocha Arsene Wenger aliwaonyesha
nyodo.
Alitaka mchezaji huyo kufanya majaribio wakati wakala
aliamini kwamba mchezaji wake hakuwa kwa ajili ya kufanya majaribio. Akaondoka
naye, wakasafiri hadi Monaco nchini Ufaransa, kule pia mambo yakawa hayohayo.
Wakala alishikilia msimamo wake hadi Zlatan aliponunuliwa na
Ajax. Leo ni kati ya wachezaji bora na matajiri. Anazeeka na mpira wake mguuni.
Utaona hapo, alichokuwa akikitaka wakala ni mafanikio ya
baadaye ya mchezaji wake. Si kiasi gani cha fedha angekipata kama Zlatan
angesajiliwa na Arsenal.
Sisemi wakala wa Msuva naye amkataze Msuva kufanya
majaribio. Badala yake lazima awe mtu ambaye amekaa chini na kiungo huyo na
kumuelewa anataka nini. Vizuri kuangalia mafanikio pia yatakuwaje kuliko kujali
watalipwa nini.
Biashara ya kuuza mchezaji, inaweza kulingana na ile ya
kuuza nyanya. Kwani nipunguzie ipo na kama ilivyo katika uuzaji nyanya
unaposema kuwa inaonekana kuharibika upunguziwe bei, hata mchezaji unaweza
kusema anatumia mguu mmoja hivyo bei yake ishuke.
Msimamo wa wakala au meneja ukoje? Msimamo huo unaendana
vipi na Msuva, naye anakubaliana nao au ana hamu tu ya kucheza soka nje ya
Tanzania na hasa Afrika Kusini bila ya kujali mambo sahihi yako vipi?
Bado Msuva hajafanikiwa kwa kuwa ndiyo ameanza majaribio.
Kufanikiwa ni jambo moja, bei na maslahi husika ni jambo jingine. Lazima
tukubaliane kwamba mtu asiye na tamaa na mzoefu ndiye anapaswa kushughulikia
suala la kiungo huyo.
Kama mtu asipokuwa mzoefu, Wazungu watampiga kwa kuwa ni
wajanja na wazoefu wa bishara hizo.
Tamaa pia ni jambo baya katika biashara ya uuzwaji mchezaji.
Kwani meneja au wakala akiwa ni mtu mwenye tamaa, ni rahisi Msuva kuuzwa katika
bei isiyo sahihi. Kumbuka Yanga walivyomuuza Nonda Shabani ‘Papii’ kwa dola
10,000 kwa Vaal Professional halafu wakaanza kujuta miaka nenda rudi.
Msisitizo, wakati yote yanafanyika. Msuva lazima ajitambue
na aachane na hofu ya kufeli pia aachane na hofu kucheza ya Afrika Kusini.
Ajiamini kwa kuijua thamani yake. Kila la kheri.








0 COMMENTS:
Post a Comment