HARAKA nianze na kuwakumbusha kwamba Tanzania tumekuwa
na wachezaji kadhaa waliowahi kucheza katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini lakini
hakuna aliyecheza kwa mafanikio makubwa.
Kama nitakuwa nimemsahau mmoja uniwie radhi lakini
nakukumbusha hawa, Nteze John alicheza QwaQwa United, Yusuf Macho ‘Musso’ (Jomo
Cosmos), Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ (Vaal Professional), Victor Costa
(Maritzburg United), Selemani Matola (Super Sport United) na sasa Mrisho Ngassa
aliyejiunga na Free State Stars iliyokuwa inajulikana kama QwaQwa United.
Utaona kuna mtiririko mdogo sana wa wachezaji wetu
kwenda kucheza Afrika Kusini, inawezekana ni ule woga wa miaka mingi au homa ya
nyumbani ambayo imekuwa ikiwasumbua wachezaji wengi wa Tanzania.
Nilimsikia Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Jerry
Muro, akihojiwa na akatumia muda mwingi kuponda kuhusiana na Ligi Kuu ya Afrika
Kusini (PSL) akiita ni ligi ya mchangani.
Ilikuwa ni siku moja baada ya Muro kusema haoni kama ni
sahihi mtu kama Simon Msuva kufanyiwa majaribio katika Klabu ya Bidvest ya
Afrika Kusini. Siku iliyofuata Mrisho Ngassa akatua katika Klabu ya Free State
Stars.
Sielewi, inawezekana Muro alizungumza kishabiki lakini
nikaona si sawa kuacha maneno yake yaende, yapite kwenye masikio na baadaye
ubongo wa wanamichezo na kuanza kuamini kuwa kweli ligi hiyo ni ya mchangani.
Sioni kama suala la Nonda Shabani aliyeuzwa na Yanga kwa
Vaal Professional ya Afrika Kusini kabla ya kupata timu nchini Uswisi ndiyo
kitu pekee ambacho Watanzania wanaweza kuona ni kizuri.
Inawezekana pia mdogo wangu Muro amekwenda Afrika Kusini
mara kadhaa, lakini hakupata kufuatilia kuhusiana na ligi hiyo na ubora wake.
Achana na kwamba wenzetu wamecheza zaidi ya mara mbili michuano ya Kombe la
Mataifa Afrika, mara moja Kombe la Dunia, lakini ni ligi yenye mfumo bora
kabisa. Viwanja vyao ni bora kuliko nchi nyingine yoyote Afrika.
Hauwezi ukalinganisha hata kidogo na ligi yetu kwa maana
ya vifaa bora na malipo bora. Hicho ndicho mchezaji anachofuata na si jina zuri
la nchi. Wanaweza wakawa hawalipi sana lakini wachezaji wanaolipwa zaidi Afrika
Kusini ni Thiko Modise wa Mamelodi Sundowns na Siphiwe Tshabalala wa Kaizer
Chiefs ambao kila mmoja kwa mwezi analamba rand 450,000 (Sh milioni 75).
Kweli Ngassa hawezi kufikia kiwango hicho kwa sasa,
lakini ana nafasi ya kupata mshahara mkubwa zaidi ya Yanga, mazingira mazuri ya
kazi na nafasi ya kuonekana kwa urahisi ikiwezekana aende Ulaya ambao
wanafuatilia PSL zaidi kuliko ligi yetu.
PSL inaongoza kwa udhamini mkubwa zaidi barani Afrika. Benki ya Absa inalipa
dola milioni 61 (zaidi ya Sh bilioni 121) kwa miaka mitatu. Runinga ya
SuperSport inalipa dola milioni 195 (Sh bilioni 387.5) kwa mwezi kwa ajili ya
fedha za haki za runinga. Timu zinafaidika, wachezaji wanafaidika.
Hauwezi kuiita PSL ni ligi ya mchangani. Inawezekana
kabisa Muro anaweza kurudi na kujifunza zaidi kwamba Afrika Kusini wana timu
bora kama Kaizer Chiefs, Orlando Pirates (iliing’oa TP Mazembe msimu uliopita),
Mamelodi na nyingine.
Hivyo, Msuva, Ngassa na wengine wakipata nafasi Afrika Kusini,
wasione wanaenda mchangani, wapo sahihi na wapambane zaidi kuvuka hapo.
0 COMMENTS:
Post a Comment