June 26, 2015


TAIFA Stars imepata bosi mpya, safari hii kwa mara nyingine ni mzawa, Charles Boniface Mkwasa ambaye ni kocha msaidizi wa Yanga.


Mkwasa atakuwa anasaidiwa na mzawa mwingine, Hemed Suleiman, maarufu kama Morocco. Sasa ni timu ya Watanzania inayoongozwa na Watanzania.

Waandishi kazi yetu kuchimba, nilizipata taarifa hizo mapema sana, kwangu ikawa ni kusubiri kama kweli TFF watakuwa na uthubutu huo wa kumrudisha mzawa katika nafasi hiyo kubwa kabisa.

Mara baada ya kutangazwa, utani kwenye mitandao mbalimbali ukaenea. Eti, Rais wa nchi-Yanga, Rais wa TFF-Yanga, Nahodha wa Taifa Stars-Yanga, bingwa wa nchi-Yanga, sasa na Kocha Taifa Stars-Yanga!

Soka lina raha yake, utani ni kitu cha kawaida, lakini mimi nikajua Mkwasa ninayefahamu utendaji wako, kamwe hauwezi kuwa na utani kwa kuwa unaelewa nini maana ya timu ya taifa.

Kamwe siwezi kupoteza muda kukufundisha kuhusiana na uzalendo, umeichezea Yanga katika michuano ya kimataifa ukiliwakilisha taifa, lakini umeichezea Taifa Stars, hivyo kwangu niseme nikaona ni uchaguzi mwafaka katika kipindi hiki.

Lakini nikaona ndiyo wakati mwingine tena wa kujifunza tukiwa na kocha mzawa kwa kuwa sasa imekuwa kitambo, makocha wageni wamekuwa wakituongoza huku “tukipigwa tu”.

Mara ya mwisho, Stars iliongozwa na mzalendo, Mshindo Msolla. Baada ya hapo, ikawa ni makocha wa kigeni kubadilishana hatua kwa hatua wakianzia na Marcio Maximo.

Maximo alitua nchini Juni, 2006 hadi sasa 2015 ni miaka tisa, hatujawahi kuwa na kocha mzawa wa kikosi cha Taifa Stars. Mkwasa unarejea tena kuwa mzawa, tena ukisaidiwa na mzawa mwingine.

Stars imepita kwa wageni kwa miaka tisa, Maximo kutoka Brazil, Jan Poulsen na baadaye Kim Poulsen kutoka Denmark na baadaye Mart Nooij (Uholanzi).

Mafanikio makubwa kama mabadiliko ambayo iliyapata Stars, ilikuwa ni kushiriki michuano ya Chan kule Ivory Coast wakati wa Maximo. Baada ya hapo, kumekuwa na mabadiliko madogomadogo sana labda kupatikana kwa wachezaji makinda na vinginevyo.

Ukiachana na hivyo, hakuna tofauti kubwa sana kwa maana ya mafanikio, labda mabadiliko kwenye sura ya timu kwa maana ya udhamini mnono ambao umekuwa ukifanya timu iweke kambi katika hoteli kubwa na bora, wachezaji wapate posho angalau nzuri, usafiri safi na viwanja vizuri vya mazoezi, hali kadhalika vifaa wanavyotumia.

Tena tumeambiwa utakuwa ukilipwa donge nono la mshahara wa dola 12,000 (zaidi ya Sh milioni 27) kwa mwezi alizokuwa akichota ‘babu’ Nooij. Unakuwa kocha wa kwanza mzawa kulipwa fedha nyingi kama hizo ukiwa na Taifa Stars.

Kitita hicho kwa mwezi si kwako wewe tu kocha, naamini hajawahi kulipwa yeyote hasa kwa wazawa katika mchezo wa soka au mingine. Maana yake kwa sasa wewe ndiye mwanamichezo ghali kuliko wengine Tanzania. Hongera kaka, ingawa nasikitika sikudai, maana huu ungekuwa muda mwafaka.

Dhumuni la barua hii ni kukukumbusha mambo mawili matatu, kwamba Watanzania wa sasa si wale wa zamani. Kweli ni wazalendo na nikuhakikishie kwamba wanaipenda sana timu yao. Hivyo lazima ukubali kuwa kweli muda unatakiwa lakini si muda mwingi wa mwendo wa kobe.

Kamwe Watanzania hawawezi kuiona Stars ikiboronga kwa miezi 12 wakakaa kimya kwa kuwa wewe ni mzawa.

Nilitamani nikunong’oneze hata nisiandike hapa. Kwamba nafasi umeipata, huenda huu ndiyo wakati mwafaka wa kuwazika kabisa makocha wa kigeni.

Mwambie Morocco kuwa mfanye kweli ili TFF na wadau wengine wawasahau kabisa makocha wa kigeni. Rungu liko mikononi mwenu, kazi kwenu mchague mpige upande upi kumaliza ‘mchezo’.

Nimesafiri nawe zaidi ya mara tatu ukiwa na Twiga Stars iliyokuwa ina maandalizi lakini haipati kila kitu, lakini ilifanya vizuri, kumbuka tukiwa Ethiopia, tulipata ushindi wa kishindo na timu ikacheza Kombe la Mataifa Afrika.

Najua unaweza, lakini changamoto zitakuwa nyingi. Wabongo wenzangu nimewashauri tukuunge mkono, lakini lazima ukubali kwamba kazi uliyonayo ni kubwa na kamwe hauwezi kuwa na visingizio.

Hauwezi kusema hatuna wachezaji, najua hauwezi kusema hatuna uwanja mzuri wala vifaa au sehemu nzuri ya kuweka kambi. Kama ni posho, waambie wawahishe wasiue morali. Halafu kamua, wamalize wageni na uzike miaka tisa ya mapito yao.

Ushauri mwingine mdogo, usikubali kuyumbishwa na Uyanga na Usimba. Angalia kilicho sahihi, fanya kwa faida ya taifa.

Kumbuka, ukishindwa wewe safari hii, basi huenda ukawa ndiyo mwisho wa wazawa kuinoa Taifa Stars kwa miaka mingine tisa ijayo au zaidi. Rungu ulilopewa ni kuipa heshima Stars na taifa letu, lakini kuwapa heshima makocha wazawa.

Mimi hata sifichi, ninakuunga mkono wewe na wote katika kikosi chako, lakini mkishindwa, mkazidi kuboronga nje ya uvumilivu, nageuza gari, kazi inaanza.

Nawatakia kila la kheri, ila nakukumbusha wewe na wenzako, maumivu ya moyo yamekuwa makubwa mno, ya muda mrefu mno, tupunguzieni.

Wako ‘pumzi pipa’

Saleh Ally

3 COMMENTS:

  1. Bado ninaamini kuwa tatizo la Stars sio kocha wala wachezaji.Hata tukimpa miaka miwili Mkwassa bado hakutakuwa na mafanikio kama hakutakuwa na mabadiliko ya kimfumo kwenye watawala wa soka.Ni lazima tubadilishe usimamizi wa soka,kwani timu ya taifa ni kielelezo cha mwisho cha jinsi gani soka linaendeshwa katika ngazi zote.Huwezi ukawa na mafanikio katika timu ya taifa wakati hakuna ligi ya maana,kanuni zinabadilishwa katikati ya msimu kuibeba timu moja,marefa wanaboronga kwa makusudi huku wengine wakiwa hawana uwezo,hakuna msisitizo wa ligi za vijana,viongozi wa FA mikoani hawatekelezi majukumu yao badala yake wanasubiri vikao ili wapate posho,nafasi muhimu katika sekretarieti na kamati za TFF wanapewa watu wasiofaa kwa sababu za kujuana,wadau wa soka kama kina Ndumbaro wanapewa adhabu za kuwapoteza kwenye ramani ya soka badala ya kuwaleta karibu ili wachangie kuendeleza soka,Viongozi hawataki kukosolewa n.k Sioni mabadiliko atakayoyaleta Mkwassa bila mapungufu haya kuondolewa,na kiukweli amepewa kazi hiyo ili kufunika kombe na mwisho wa siku TFF wapate nafasi ya kubeza makocha wazawa

    ReplyDelete
  2. Katika nchi ambayo kocha bora wa msimu wa ligi kuu ni yule ambaye hakuandaa timu wakati ligi inaanza au duru la pili linaanza,golikipa bora hakuwa na timu kwa sehemu kubwa ya ligi,ratiba ya ligi inabadilika kila siku na timu nyingine zinacheza mechi zote mbili katika mzunguko mmoja wa ligi,ligi ,hivi unatarajia kocha wa timu ya taifa afanye miujiza gani?unatarajia wachezaji wa timu ya taifa wafanye miujiza gani?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic